Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MKURUGENZI Ofisi ya Rais Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Firimin Msiangi amezitaka Taasisi zote za serikali kuhakikisha zinateketeza nyaraka za serikali kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo ya uteketezaji wa nyaraka hizo.
Akizungumza leo Juni 19,2024 jijini hapa katika banda la Idara hiyo kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma alisema nyaraka hizo ni za siri hivyo zinatakiwa zionwe na mtu husika na kwamba wakati wa uteketezaji wake lazima uzingatie sheria na taratibu zilizopo.
Akielezea kuhusu majukumu ya ofisi yake amesema, moja ya majukumu ya ofisi hiyo ni kutunza nyaraka za serikali huku akisema katika Idara yao kuna nyaraka yenye mawazo ya Makao Makuu kuhamishiwa Dodoma ambapo amesema nyaraka hiyo ipo tangu enzi za mkoloni.
Amesema kuwa vmaamuzi yote ya serikali yanahifadhiwa vyema kwa ajili ya rejea mbalimbali, kutunga na kufanya mabadiliko katika uendeshaji wa nchi.
” Kwa kweli kumekuwa na mafanikio makubwa katika kuhakikisha nyaraka za serikali zinazalishwa, zinahifadhiwa zinatunzwa kwa muda mrefu, ofisi yangu ndio yenye dhamana hii.”amesema Msiangi
Aidha amesema mwaka 2002 ilitungwa Sheria nyingine na Bunge iliyolenga kuiongezea nguvu Idara hiyo ambapo iliongezewa majukumu ya kusimamia mifumo ya uzalishaji wa nyaraka hizi zinazotumika katika ofisi za serikali kwa maana kumbukumbu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msiangi mwaka 2004 pia Idara hiyo iliongezewa jukumu jingine la kuhakikisha nyaraka zinazozalishwa na viongozi wa Kitaifa Mwalimu Nyerere na Amani Abeid Amani Karume kuhakikisha nyaraka zao zinazowagusa zinakusanywa vizuri na zinahifadhiwa kwa ajili ya urithi andishi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema taasisi hiyo ilianza mwaka 1963 chini ya waraka wa Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeelekeza iundwe kwa ajili ya nyaraka za serikali lengo likiwa ni kuhakikisha nyaraka hizo zinazalishwa, zinatunzwa zinateketezwa na kuhifadhwa vizuri ili kutunza historia na urithi anzishi wa nchi.
Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa mwaka 1965 ilitungwa Sheria na Bunge ambapo Sheria ya nyaraka namba 33 ilianzishwa ikiipa nguvu waraka wa Rais wa awamu ya kwanza ambapo kazi yake ni ile ile ambapo sasa ni kukusanya, kuzalisha kuhifadhi na kuteketeza nyaraka za serikali kwa mujibu wa taratibu.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa