November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyamoga: Kilolo msifanye makosa Oktoba 28

Na Zuhura Zukheir, TimesMajira Online, Iringa

KUELEKEA uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu, Mgombea Ubunge Jimbo la Kilolo mkoani Iringa, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Justin Nyamoga, amewaomba wananchi wa jimbo hilo kuchagua viongozi wenye maono ya kuwasaidia kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani ili waendeleze kazi nzuri zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano

Nyamoga ameyasema hayo wkatika uzinduzi wa kampeni za udiwani kata ya Ilula na kusema, wananchi wanatakiwa kuacha majaribio katika kuchagua viongozi na kuacha tabia ya kuchagua kwa ushabiki wa vyama, hivyo wanatakiwa kusikiliza sera za wagombea wenye ilani na sio wale wanaoenda kukejeli na kutoa lugha za matusi kwa serikali iliyokuwa madarakani

“Ndugu zangu acheni kufanya majaribio katika kuchagua viongozi kata hii ya Nyalumbu na Ilula mwaka 2015 mlifanya makosa makubwa kuchagua madiwani wa upinza na madhara yake mmeyaona maana ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa maendeleo, hamkuwa na mtu sahihi wakuwasemea” amesema Nyamoga.

Hata hivyo Nyamoga amesema, wananchi wanatakiwa watambue wanapo mpigia kura diwani, mbunge na Rais wa CCM, kura hizo wanakuwa wamewakopesha na wanatakiwa kuwalipa juu ya maendeleo ndani ya kipindi cha miaka mitano, hivyo umakini unahitajika wakati wa kupiga kura wahakikishe wagombea watakao wapigia kura waeleze nini watawafanyia mkiwachagua

Naye mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) Terresia Mtewele amesema, bado matumani makubwa ya wananchi Tanzania yapo ndani ya CCM kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli .

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdalah amesema, serkali imeimarisha ulinzi katika kipindi chote cha kampeni na haitafumbua macho viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani utakaofanywa na wafuasi ama viongozi wa chama vhochote.