Na Iddy Lugendo, timesmajiraonline
MKUU wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo amefungua semina kwa waajiri wa sekta binafsi iliyoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Temeke, Dar es Salaam yenye lengo la kuwakumbusha majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuwasilisha michango kwa wakati.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo leo julai 19, 2022 Ilala, jijini Dar es salaam mkuu wa wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo amewapongeza na kutoa wito kwa ‘NSSF’ kuendelea kukutana na waajiri kwa sababu fursa hiyo inatoa nafasi yakutatua changamoto mbalimbali na kukumbushana majukumu ya kila moja.
Katika semina hiyo mada mbalimbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na shughuli za Mfuko, Maboresho ya kanuni ya kikokotoo na Maboresho ya Mfumo wa Usajili na Uwasilishaji wa Michango kwa upande wa waajiri(employer portal) na huduma za mifumo kwa wanachama
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Cosmas Sasi amewashukuru waajiri wa sekta binafsi kwa kushiriki semina hiyo ambapo pia amewataka kutimiza wajibu wao wa kuwasilisha michango na kuwasajili wanachama wapya kwa mujibu wa Sheria.
Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke
Feruzi Mtika amewashukuru waajiri kwa namna wanavyoshirikiana na Mfuko jambo ambalo limechangia mafanikio ya NSSF ambapo katika mwaka wa fedha uliopita Mfuko katika Mkoa wa Temeke ulikusanya shilingi bilioni 217 na kuandikisha asilimia 60 ya wanachama.
Naye, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF Lulu Mengele, amesema Mfuko unaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ambao wanafanya shughuli kwenye sekta binafsi na makundi mbalimbali ili kuongeza uelewa wa hifadhi ya jamii.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato