November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NSSF yabainisha mafanikio lukuki

-Mkurugenzi mkuu abainisha mafanikio lukuki, amesema yamechangiwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

-TEF yakoshwa na utendaji wa NSSF yapongeza kazi kubwa inayofanywa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Ni funga kazi pengine unaweza kusema hivyo! Baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba kubainisha mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Mfuko katika kipindi cha Machi 2021 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023.


Mshomba amesema hayo tarehe 25 Septemba, 2023 jijini Dar es Salaam, wakati akitoa wasilisho la utekelezaji wa majukumu ya NSSF kati ya Machi 2021 hadi Juni 2023 kwenye kikao kazi baina ya Mfuko, wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Amesema NSSF imefanikiwa kuandikisha wanachama wapya 547,882, kati ya tarehe 1 Machi 2021 na 30 Juni 2023 na kwamba idadi ya wanachama wachangiaji iliongezeka kwa asilimia 36 kutoka 874,082 tarehe 1 Machi 2021 hadi kufikia wanachama 1,189,222 tarehe 30 Juni 2023.

“Siri ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na mkakati wa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sera nzuri za kuvutia wawekezaji, pamoja na utekelezaji wa mpango wa Mfuko katika uandikishaji wanachama na matumizi ya TEHAMA,” amesema.

Kuhusu makusanyo ya michango amesema katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023, kwa mwezi yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 97.67 iliyofikiwa tarehe 1 Machi 2021 hadi kufikia TZS bilioni 143.05 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023.

Hata hivyo, amesema makusanyo ya michango kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 43 hadi kufikia shilingi bilioni 1,718.28 katika mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 1,201.05 zilizokusanywa katika mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2021.

Amesema uwekezaji wa Mfuko pia uliongezeka kwa asilimia 111 kutoka shilingi bilioni 3,395.46 tarehe 1 Machi 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 7,153.23 tarehe 30 Juni 2023. Kati ya mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2021 na mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2023, thamani ya vitega uchumi vya Mfuko imekua kwa asilimia 55 hadi kufikia shilingi bilioni 7,153.23 tarehe 30 Juni 2023 kutoka shilingi bilioni zilizokuwa tarehe 30 Juni 2021.

Mshomba amesema katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023, NSSF ilitumia wastani wa shilingi bilioni 61.93 kwa mwezi kulipa mafao mbalimbali kwa wanachama na wategemezi ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ukilinganisha na wastani wa shilingi bilioni 50.58 kwa kipindi kilichoishia tarehe 1 Machi 2021.

Aidha, kati ya mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2021 na mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023 malipo ya mafao yaliyolipwa kwa wastaafu, wanachama na wanufaika wengine yaliongezeka kwa asilimia 25 na kufikia shilingi bilioni 743.17 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023 ukilinganisha na bilioni 594.33 zilizolipwa Juni 30, 2021.

Kuhusu Mpango wa Taifa wa Sekta isiyo Rasmi (NISS), Mshomba amesema Mfuko umefanya mapitio ya Mpango wa utoaji wa huduma za Hifadhi ya Jamii katika sekta isiyo rasmi (NISS).

Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deusdatus Balile amepongeza mafanikio mbalimbali ya NSSF yakiwemo ya ongezeko la michango, ongezeko la wanachama wachangiaji, ongezeko la mapato pamoja na ulipaji wa mafao.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, akizungumza katika kikao kazi kilichoratibiwa kati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)  na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kilichoanza tarehe 1 Machi 2021 hadi Juni 30, 2023 ambapo amesema NSSF imepata mafanikio kwa upande wa uandikishaji wanachama, ukusanyaji michango, uwekezaji na kulipa mafao.
Kikao kazi hicho na wahariri wa vyombo vya habari kimefanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC), Dar es Salaam, tarehe 25 Septemba 2023 chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Wakurugenzi kutoka Kurugenzi mbalimbali pamoja na baadhi ya Mameneja wa NSSF wakifuatilia kwa makini mkutano wa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba (hayupo pichani) na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. Mkutano huo umefanyika tarehe 25 Septemba 2023, katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC), Dar es Salaam.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele akitoa neno la utangulizi katika mkutano wa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambao umefanyika tarehe 25 Septemba 2023, katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC), Dar es Salaam.

Matukio katika picha wakati wa mkutano wa wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina.