Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online
BENKI ya NMB imekuwa taasisi ya kwanza kutekeleza rasmi mpango wa bima ya afya kwa wakulima nchini baada ya kuingia makubaliano ya kutoa huduma hiyo na vyama vikuu viwili vya ushirika mkoani Tabora.
Kwa kuanzia, NMB imetenga zaidi ya Sh.bilioni 5 kwa ajili ya kuwakopesha wakulima chini ya utaratibu wa Ushirika Afya
Utiaji saini wa makubaliano hayo na vyama vya wakulima wa zao la tumbaku yanayouhusisha pia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulifanyika Ijumaa iliyopita kama sehemu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ushirika iliyoazimishwa kitaifa Tabora.
Vyama hivyo ni WETCU na Mirambo vinavyowakilisha vyama vidogo vya wakulima zaidi ya 200 mkoani humo. Kupitia mpango wa Ushirika Afya wanachama wa vyama hivyo wapewa mikopo isiyo na riba na Benki ya NMB kwa ajili ya gharama za matibabu kwa kutumia kadi za NHIF.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amedhibitisha kuanza rasmi kutolewa kwa huduma hiyo baada ya kuwakabidhi kadi za NHIF wanufaika watatu wa mpango wa Ushirika Afya kwenye kilele cha Siku ya Kimataifa ya Ushirika Jumamosi iliyopita.
Katiba hotuba yake ya kuadhimisha siku hiyo na kabla ya kukabidhi kadi hizo, Waziri Mkuu alizishukuru taasisi za fedha kwa mchango wake wa kuviimarisha vyama vya ushirika na kuvifanya kuwa nguzo muhimu ya kiuchumi.
“Sisi kama serikali tunaridhika na mchango wa taasisi za fedha kuusaidia ushirika. Pia tumezishawishi benki kuliangalia swala ra riba na zimekubali kulishughulikia na sasa ufumbuzi wake unatafutwa kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania,” amesema.
Kadi za NHIF zilizofadhiliwa na NMB zilizotolewa na Waziri Mkuu kwa wakulima wa tumbaku Kulwa Mfaume, Saleh Mpemba na Athanas Semeduke ni miongoni mwa kadi 102 za kwanza ambazo zimetolewa na benki hiyo na kuifanya kuwa ya kwanza kufanya hivyo.
Aidha, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Bw Filbert Mponzi, alisema wana mpango wa kuongeza kiasi cha pesa kwa ajili ya mikopo ya wakulima ya bima ya afya.
“NMB tumetenga zaidi ya TZS bilioni 5 kwa ajili ya kukopesha wakulima zaidi ya 300,000 kupata bima ya afya ambayo haina riba kabisa. Kiwango hiki kitaongezeka kutokana na mahitaji na muitikio wa wakulima,” kiongozji huyo alidokeza kabla ya kutiwa saini za makubaliano na vyama vikuu vya tumbaku.
“Tukio la leo ni faraja kubwa kwangu, na kwa Benki ya NMB kama mdau mkubwa wa Serikali na kama benki inayohudumia zaidi ya Watanzania milioni nne nchi nzima, mpango huu utahakikisha urahisi wa kupatikana kwa bima ya afya kwa wakulima wote wa tumbaku wa Tabora na mazao mengine nchi nzima,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Bw Mponzi, pamoja na kuchochea kilimo chenye tija, sababu kubwa ya NMB kuwekeza katika mpango wa Ushirika Afya ni kuunga mkono juhudi za serikali katika jitihada zake za kufikia malengo ya Afya kwa Wote kupitia bima ya afya.
Pia amesema kuwakopesha wakulima bila riba yoyote na kuwapa nafasi ya kufanya marejesho baada kuuza mazao yao ni kutambua mchango wao mkubwa katika ujenzi wa taifa na kuwa wateja wazuri wa NMB.
Mkuu wa Kilimo Biashara wa benki hiyo,Issac Masusu, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wiki hii kadi nyingine 90 za NHIF kwa ajili ya Ushirika Afya zitatolewa kwa wakulima wa Kahama.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw Bernard Konga, amesema kuwa mpango huo ulianzishwa mwaka 2018 lakini utekelezaji wake ulidororo kutokana na changamoto ya vipato vya wakulima ambayo sasa imetatuliwa na ufadhili wa NMB.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Udhibiti na Usimamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, alisema ufadhili wa aina hiyo unaviongezea vyama vya ushirika thamani na utasaidia kuwashawishi wakulima wengi kujiunga navyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Barozi Batilda Buriani, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Bw Louis Bura, amesema bila ya baraka na udhamini wa TCDC zoezi hilo lisingefaulu kwa kiwango cha sasa hivi.
“Utaratibu huu unarahisisha kazi yetu ya kuwahamasisha wakulima kijiunga na vyama vya ushirika na utaongeza idadi ya watu wenye bima za afya kama serikali hii inavyotaka na kuelekeza,” Bw Bura alifafanua.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi