December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yatoa rai kwa AMCOS kuelekea msimu mpya malipo ya korosho

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KUELEKEA msimu mpya wa mauzo ya Zao la Korosho 2020/2021 Benki ya NMB imewataka viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika AMCOS wa mikoa ya kanda ya kusini ambayo inazalisha zao hilo kuhakikisha wanaandika majina sahihi ya wakulima pamoja na akauti namba zao kwa usahihi.

Benki hiyo imesema kuwa kuandikwa kwa usahihi majina na namba za akaunti, itaondoa usumbufu wa fedha kushindwa kuingizwa kwenye akauti ya mkulima ikiwa pamoja na kutokuwepo kwa malalamiko ya ucheleweshwaji wa malipo.

Rai hiyo imetolewa jana na Meneja Benki hiyo Kanda ya Kusini Janeth Shango wakati akizungumza na Wafanyabiashara na wateja wa benki hiyo kwenye jukwaa la klabu ya Wafanyabiashara (BUSINESS CLUB) wa Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Janeth amesema katika msimu uliopita wa mwaka 2019/2020 walikutana na changamoto ya fedha kushindwa kuingia kwenye akaunti za wakulima kwa wakati kutokana na majina ya akaunti kutofautiana na majina ya wakulima na baadae kupelekea baadhi ya wakulima kulalamika kucheleweshewa malipo yao.

“Ili kuondokana na changamoto hii tayari tumetoa elimu kwa viongozi wa AMCOS pale ambapo wanawaandikisha wakulima wahakikishe wanaandika jina sahihi la mkulima pamoja na akaunti namba yake ikiwezekana amuonyeshe kadi yake ili aweze kuandika namba na jina lake kama lilivyopale”…….

“ ..lakini mbali na hiyo tumekubaliana na viongozi wa AMCOS kuleta majina ya malipo yao kabla ili yaweze kufanyiwa uhakiki ambapo zoezi hilo tumesha lianza hivyo kwa msimu huu hatutegemei tena kukutana na changamoto ya pesa kushindwa kuingizwa kwenye akaunti ya mkulima tena” alisema Shango

Hata hivyo Shango amesema kuwa NMB imejipanga katika msimu huu wa malipo kuhakikisha huduma zinakwenda kwa haraka hasa malipo ya wakulima kuwafikia kwa wakati ambapo benki hiyo imeongeza watoa hudma katika matawi yake kwa mikoa yote.

Amesema ili kuondoa msongamano mkubwa kwenye Matawi yao wao kama benki tayari wamefanya mafunzo kupitia majukwaa mbali mbali ya kuwakutanisha Mawakala wote wa NMB Wakala ya kuwajengea uwezo wa namna ya kuwahudumia wakulima hao kwa karibu zaidi

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Athari za mikopo ‘Head of Credit Risk’NMB Oscar Nyirenda amewataka wakulima na wateja wa benki hiyo hiyo kuanza kutumia huduma ya bima ambayo NMB imeanza kuitoa ili kuweza kujilinda na majanga mbali mbali wanayoweka kukutananayo katika shughuli zao za kujikwamua kiuchumi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa ambae alikua mgeni rasmi katika kongamano hilo, aliipongeza benki ya NMB kwa kuamua kukutana na wafanyabiashara jambo ambalo linaonesha namna benki hiyo inavyowajali wateja wao.

Baadhi ya wafanyabishara wakapongeza huduma za bima ambazo zimeanza kutolewa na benki hiyo kupitia matawi yake yote nchi nzima,ambapo walisema kuwa imewarahishia upatikanaji wa huduma hiyo.

“Huduma ya Bima ni muhimu sana kwa sisi wafanyabiashara, mfano vyombo vya moto muda wote vipo barabarani, unaweza ukapata ajali, unaweza ukagonga unaweza ukaanguka, kwahiyo ukikata bima ya chombo chako unarejeshewa, kulingana na bima uliyokata.” alisema Mwanahiza Mdee ambaye ni mfanyabiashara.