Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
NMB na Klabu ya Simba wamezindua ushirikiano wa kibiashara uitwao ‘Ukaribu wa Nguvu’ kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kufanya usajili wa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Simba, Imani Kajula, amesisitiza kuwa lengo la Ukaribu wa Nguvu ni kuwafanya wadau wa Simba washabikie timu yao kwa faida zao.
Ukaribu wa Nguvu ni mfumo ambao unajumuisha akaunti tatu za benki ya NMB: NMB Simba Account, NMB Simba Queens Account (kwa wanawake), na NMB Simba Mtoto Account (kwa watoto). Mashabiki na wanachama wa Simba watapata huduma hizi kwa kujisajili kupitia mtandao wa matawi 229 ya NMB.
Kadi za akaunti hizo zitakuwa na Bima ya Maisha ya hadi Sh. Mil. 6.Uzinduzi wa ushirikiano huo ulifanyika Jumamosi kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Simba, ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti Murtaza Mangungu, na wawakilishi wa NMB, ikiwa ni pamoja na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Filbert Mponzi, Afisa Mkuu wa Biashara ya Kadi Philbert Casmir, na Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi Donatus Richard.
Katika uzinduzi huo, Filbert Mponzi alisema kuwa ushirikiano huo utawanufaisha wote, hususani mashabiki wa Simba, ambao wataweza kupata huduma za benki kama vile Mshiko Fasta – mikopo nafuu isiyo na masharti kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo.
Aidha, Imani Kajula aliongeza kuwa kadi hizo za NMB zitawawezesha mashabiki wa Simba kufanya miamala na pia kupata ofa za mapunguzo ya asilimia 10 na kuendelea watakapolipia huduma kupitia kadi hizo.
Kwa upande wake, Murtaza Mangungu alieleza kuwa ushirikiano huo na NMB utasaidia katika kuendesha timu, kusajili wachezaji wazuri, na mambo mengine ya klabu.
Hivyo, aliwataka mashabiki ambao walikuwa na kadi za taasisi nyingine za kifedha kuhama na kujiunga na NMB.
Ushirikiano huu na NMB unafuatia makubaliano kama hayo yaliyofikiwa kati ya NMB na klabu nyingine ya soka Tanzania, Yanga.
Hafla hiyo pia ilishuhudia utambulisho wa mchezaji mpya wa Simba, Willy Essomba Onana kutoka Cameroon, na tarehe za uzinduzi wa jezi mpya zilizopangwa kufanyika Julai 21 kwenye Mlima Kilimanjaro, na Tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 6.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba