Na, Mwandishi wetu, TimesMajira Online
BENKI ya NMB imeingia Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Kampuni ya Uuzaji na Usambazaji Gesi ya Oryx Gas Tanzania, yaliyopewa jina la ‘Moto Mkali Bei Poa’, ambao ni mpango mkakati unaolenga kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ya kupikia, ili kuunga mkono juhudi za utunzaji mazingira kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dar es Salaam Novemba 26, ambako NMB iliwakilishwa na Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, huku Oryx Tanzania ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Benoit Araman, mbele ya Mkuu wa Idara ya Rasirimali Watu Oryx Energies, Kanda ya Afrika Mashariki, Loveness Hoyange..
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mponzi alisema utunzaji mazingira ni agizo lililopewa msisitizo na Benki hiyo kinara kwa suluhishi mbalimbali za kifedha na kijamii, wanajisikia fahari kusaini makubaliano hayo, yanayoenda kuwapa urahisi wa upataji gesi kwa mikopo ya riba nafuu na punguzo la bei.
“Makubaliano haya yanaakisi dhamira ya dhati tuliyonayo NMB katika utunzaji wa mazingira, eneo ambalo wiki jana tulizindua kampeni ya kitaifa ya ugawaji mizinga ya nyuki kwa vikundi vya wafugaji nchini, ikifuata nyayo za ile kampeni ya mapema mwaka huu ya upandaji miti milioni moja kote nchini, ambayo tunatarajia kukamilisha kama tulivyopanga.
“NMB tunatambua, kujali na kuthamini utunzaji wa mazingira kwa ustawi wa kizazi cha sasa na cha baadaye, ndio maana tukaja na Kampeni hii ya Moto Mkali, Bei Poa, lengo likiwa ni kuhamaisha wateja wetu kuungana na Serikali katika kumaliza changamoto ya uharibifu wa mazingira.
“Kupitia kampeni hii, tunaenda sio tu kukopesha wateja wetu mikopo ya ununuzi wa gesi na kunufaika na punguzo la bei wataponunua kwa njia za malipo ya kadi na yale ya kidijitali kwa maana ya Lipa Mkononi, bali tumeangalia mnyororo mzima wa thamani unaowajumusiha wauzaji, ambao nao watakopeshwa fedha za kuongeza bidhaa katika vituo vyao vya mauzo,” alisema Mponzi.
Kwa upande wake, Araman, alitambia mashirikiano hayo baina yao ambao ni vinara wa huduma za nishati mbadala na NMB wanaoongoza sekta ya fedha nchini, na kwamba ukongwe wao katika masuluhisho ya kifedha, unawapa uhakika wa mafanikio katika vita waliyoshiriki kwa miaka mingi ya mabadiliko ya tabianchi.
“Sisi ni wakongwe katika utunzaji wa mazingira kwa kusambaza na kuuza nishati mbadala mbadala, lengo likiwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alitoa agizo la kuhakikisha hadi mwaka 2030, tunatokomeza uharibifu wa mazingira na kila Mtanzania awe anatumia gesi ya kupikia na sio mkaa au kuni, ambazo ni hatari pia kwa afya.
“Tumekuwa watoa huduma wa muda mrefu zaidi barani Afrika na Tanzania ikiwa sehemu ya wanufaika wa huduma zetu na tunaamini katika ushirikiano huu na NMB, utaenda kuwa chachu ya ufanisi wa mpango mkakati wetu wa kuhakikisha tunawapa wateja wetu suluhisho la kupata nishati bora ya kupikia kwa ukaribu, uharaka na unafuu mkubwa.
Awali, Mkuu wa Biashara ya Kadi wa NMB, Philbert Casmir, alisema Moto Mkali, Bei Poa ni kampeni inayodhihirisha dhamira yao katika kuhakikisha wanagusa maisha ya wateja wa benki yake, na kuwa hiyo ndio siri ya makubaliano hayo, ambayo yatatoa mchango mkubwa katika utunzaji mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Kupitia malipo ya kidijitali kwa maana ya Lipa Mkononi, QR Code na Vituo vya Mauzo (PoS), wateja wa NMB wanaenda kunufaika sio tu na manunuzi ya gesi kwa njia ya kadi na kuachana na matumizi ya pesa taslimu, bali wataingia moja kwa moja droo zetu za Kampeni inayoendelea ya MastaBata Halipoi, inayotoa zawadi hazi za Shilingi Milioni 350,” alibainisha.
Naye Meneja Mauzo wa Oryx Tanzania, Shaban Mohamed, alisema Moto Mkali, Bei Poa utajikita katika maeneo ununuzi wa haraka wa Oryx Gas utakaoambatana na unafuu wa bei, Uwezeshaji wa Wasambazaji, Wauzaji wa Maduka ya Oryx pekee (Oryx Exclusive Shops), Punguzo la Bei kwa Wanunuzi wateja wa NMB na mikopo yenye riba nafuu kwa wateja wote.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza