Penina Malundo, Timesmajira
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),kimesema kuwa kinatumia sherehe ya maadhimisho ya miaka 50 ya uanzishwaji wa mafunzo ya ufundi stadi na miaka 30 ya Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kunadi kazi mbalimbali zilizofanywa na wanafunzi wa chuo chao ambazo zinaonyesha kielelezo cha jinsi ambavyo chuo hicho kimeshiriki kutoa mafunzo ya ujuzi.
Akizungumza hayo jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari katika sherehe hizo,Mkuu wa Chuo cha NIT, Dk. Prosper Mgaya amesema kazi zinazonadiwa katika maonesho ni za wahitimu wa Shahada ya Uhandisi Mitambo.
Amesema kuwa kazi hizo za wanafunzi hao zimetokana na jitihada za chuo kuhakikisha kwamba wanapata ujuzi zaidi utakaowawezesha kufanya vitu vizuri mbele ya jamii kwa ujumla.
“Kazi za vijana wetu ambazo wamezileta hapa ni za ujuzi zaidi, katika kuadhimisha miaka 50 ya uanzishwaji wa mafunzo ya ufundi stadi sisi NIT tumeonyesha jinsi ambavyo tunashiriki kutoa mafunzo ya ujuzi,” amesema
Aidha amesema chuo chao kinaendelea kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa na kwamba kazi zilizoletwa na vijana wao katika maadhimisho hayo ni zile zenye ujuzi zaidi ambazo ndizo zitamfanya pindi anapomaliza masomo kuajiriwa au kujiajiri.

Kwa upande wake Mbunifu wa Chuo hicho,Iman Dastani amesema yeye amebuni kitimwendo kinachojiendesha chenyewe kwa kutumia simu au umeme ambacho
kinaweza kufanya kazi kupitia simu ya mkononi kukiendesha hasa kwa mtu mwenye ulemavu wa viungo.
“Kiti hiki unaweza ukakichaji kama simu halafu unakitumia, kinaweza kukaa masaa manane hadi tisa kwahiyo mgonjwa au mtu mwenye ulemavu anaweza kujiendesha mwenyewe au akaendeshwa na mtu mwingine kwa kutumia simu yake,” amesema Dastani.
More Stories
MUWSA yatekeleza agizo la Rais Samia, yafunga mita za maji za ‘Prepaid’ 460
ETDCO wakamilisha mradi wa Kilovolti 132 Tabora – Urambo
Mgodi unaomilikiwa na Wakinamama wachangia Shilingi Milioni 800