January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Bodi ya NICOL, Dk. Gideoni Kaunda

NICOL kulipwa mil.580/- baada ya kushinda kesi

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dar

KAMPUNI ya NICOL imeshinda kesi ya mkopo wa sh. milioni 580 iliyokomboa kwa ajili ya kampuni ya Twiga Feeds Limited inayojihusisha na biashara ya kuku, iliyopata kutoka kwa Mfuko wa Jamii (SATF).

Wakili na Mwanasheria wa NICOL,  Benjamin Mwakagamba

Hiyo inafuatia uamuzi wa Mahakama Kuu Division ya Ardhi iliyotoa baada ya Kampuni ya NICOL, ambaye ni mlalamikiwa, kupinga madai yaliyotolewa na kampuni ya Twiga Feeds Limited na Abcon Chemicals Limited, walalamikaji, kwenye shauri husika.

Jaji Elinaza Luvanda ameiziamuru kampuni mbili zinazolalamika kulipa kiasi cha milioni sh.580 pamoja na riba yake kwa kampuni inayolalamikiwa baada ya kutupilia mbali kesi ya madai na nafuu zilizokuwa zikitafutwa, akisema walalamikaji walishindwa kuithibitishia mahakama baada ya kutoa ushahidi wao.

“Kampuni inayolalamikiwa ina haki ya kulipwa sh. milioni 580 pamoja na riba ya asilimia 18 kwa mwaka kuanzia mwaka 2009. Shauri la msingi linatupiliwa mbali na madai kinzani yameshinda,” amesema Jaji Luvanda.

Kwenye shauri hilo, walalamikaji walikuwa wameiomba Mahakama Kuu kutamka kwamba kiasi cha sh. milioni 580 zilizolipwa na mlalamikiwa kwa SATF kilikuwa mchango wa NICOL kwenye mradi wa pamoja wa uwekezaji na kwamba haukuwa mkopo.

Wameiomba mahakama kutamka kwamba kushindwa kwa mradi wa pamoja wa uwekezaji kulisababishwa na mlalamikiwa mwenyewe na kwamba riba na adhabu zinazosemwa zinatokana na fedha dhidi ya walalamikaji ni batili na hazikuwepo na kwamba Sh580 milioni zilizolipwa na mlalamikiwa hazikutakiwa kurejeshwa.

Aidha, walalamikaji waliiomba mahakama itamke kwamba mali iliyokuwa imewekwa rehani kwenye kiwanja eneo la Viwandani Mbezi, Dar es Salaam, ilikuwa imefanywa kwa udanganyifu na ilikuwa batili na kwamba wanaiomba mahakama itamke kwamba iachiwe.

Kwa upande mwingine, mlalamikiwa kwenye maelezo ya utetezi wake wa kimaandishi, kupitia wakili wake Benjamin Mwakagamba, kwenye madai kinzani anaiomba mahakama kutoa uamuzi na kuwaamru walalamikaji walipe kiasi cha sh. 2,403,123,177, ikiwa ni kiasi ambacho kilikuwa hakijalipwa pamoja na riba ya mkopo.

Katika hukumu yake, Jaji Luvanda alikataa ombi la walalamikaji kwamba fedha hizo hazikuwa mkopo uliotolewa, bali zilikuwa zimetolewa na mlalamikiwa kwa ajili ya mradi wa pamoja kuhusiana na kuanzishwa kwa taasisi ya elimu ya juu, iliyoitwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (U-TAN).

Baada ya kupitia ushahidi uliotolewa, Jaji Luvunda alisema kwamba ushahidi wa walalamikaji haukuwa dhahiri juu ya jambo la msingi na hakuna mahali popote kwenye barua ya mlalamikiwa ilipoandikwa kuhusu chuo kikuu na kwamba hakuna anayejua kama ilifanywa hivyo makusudi au kwa kukosa uangalifu.

“Kwa hiyo, hoja ya walalamikaji kwamba kulikuwa na mpango wa mradi wa pamoja wa kuanzisha chuo kikuu inakosekana,” Jaji amesema. Hivyo, alichukua msimamo sahihi kwamba kiasi cha fedha Sh580 milioni ikilichotolewa na mlalamikiwa ulikuwa mkopo.

Januari 27, 2001, Kampuni ya Twiga Feeds ilipata mkopo wa sh. milioni 580 kutoka SATF, uliotolewa kwa stakabadhi ya mkopo kwa mali zote za kampuni na kwenye tozo ya kwanza kwenye mali iliyopo eneo la Viwandani Mbezi, Dar es Salaam, na mali hiyo ya rehani ilikuwa imesajiliwa na Msajili wa Hati Machi 8, 2001.

Walalamikaji walishindwa kulipa mkopo na kuzuia chukuliwa mali iliyowekwa rehani kwa kushindwa kulipa mkopo kwa wakati uliokubaliwa, walimwendea mlalamikiwa wakipendekeza kuanzisha mradi wa pamoja wa taasisi ya elimu ya juu kwenye kiwanja cha eneo la Mbezi.

Walalamikaji walichelewesha ulipwaji wa deni, jambo lililofanya SATF kutoa notisi ya siku arubaini kwa lengo la kutumia mali iliyowekwa rehani.

Mradi wa kuanzisha taasisi ya elimu ya juu uliachwa baada ya kutolewa mkopo wa SATF na Kampuni ya Abcon Chemical Limited ilitakiwa kurejesha sh. milioni 580 kwa Kampuni ya NICOL pamoja na riba ya asilimia 18 kwa mwaka.

Bodi ya Kampuni ya Abcon Chemical Limited iliazimia kwamba kiwanja cha eneo la Viwandani Mbezi kitumike kulipa deni na Kampuni ya Twiga Feeds kwa Kampuni ya NICOL na azimio lilionyesha dhahiri kwamba iwapo kutakokea kushindwa kulipa deni mlalamikiwa atakuwa na haki ya kutumia hati kugharimia kiasi kinachodaiwa.