January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ni wajibu kwetu kuwakumbuka na kuwathamini wenye mahitaji-Othaman

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameeleza haja ya kuwakumbuka na kuwathamini wanyonge na wahitaji wa kusaidiwa katika jamii, kama sehemu ya muendelezo wa mafunzo ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Othman ameyasema hayo leo, katika Kijiji cha Kengeja, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, akisalimiana na viongozi na wananchi mbali mbali, kama sehemu ya muendelezo wa Ziara yake Maalum ya Siku Nne, kisiwani hapa.

Amesema kuwa ili kuonyesha thamani na heshima yao, ni vyema kuwafikiria na kuwatembelea watu wenye mazingira magumu wakiwemo wazee wasiojiweza, wagonjwa na watu walioondokewa, hali ambayo pia inazidisha mapenzi na mahusiano mema katika jamii.

“Tukiwathamini na kuwafikia watatuheshimu na kutupenda sambamba na kupata radhi zake Mwenyezi Mungu”, amesisitiza Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo–Zanzibar.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Masoud, amesema kuwa wananchi wake wanafarijika sana kuona Viongozi wao wanawakumbuka kwa hali na mali, hasa katika Msimu huu wa Kheri, na kwamba huo ni utamaduni wa kipekee unaohitaji kuenziwa katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika ziara yake hiyo, Mheshimiwa Othman ambaye amejumuika na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Jamii, Masheha wa baadhi ya Shehia, Vyama vya Siasa, na Vikosi vya Ulinzi na Usalama akiwemo Katibu wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kusini Pemba, Maalim Saleh Nassor, alizuru pia katika vijiji vya Ole Kipangani, Wawi Kichangani, Vitongoji, Kiwani Mtangani, Chonga Chanjamjawiri, Kimbuni, Matuleni,Chanjaani na Mkoani vyote vya kisiwani Pemba.

Aidha jioni hii, Othman amejumuika na Viongozi na Wananchi mbali mbali katika Iftari aliyoiandaa, ambayo imefanyika katika Viwanja vya Kufurahishia Watoto, Tibirinzi, Chake Chake Pemba.