November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ni miaka mitatu ya mafanikio ya Samia Wizara Mambo ya Nje

*Waziri Makamba ayaanika Bungeni, ataja vipaumbele vya Wizara, Diaspora kupatiwa hadhi maalum, uhusiano wa kidiplomasia waimarika

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuimarisha uhusiano baina ya ya Tanzania na nchi mbalimbali, taasisi za kikanda na kimataifa na kuliletea heshima kubwa Taifa.

Katika kipindi chake cha miaka mitatu ya uongozi wake, Rais Samia ametumia diplomasia kwa umahiri wa hali ya juu kulinda na kutimiza malengo ya kiuchumi ya taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jijini Dodoma, jana.

Aidha, katika hutuba yake waziri, Makamba ameanika pamoja na mambo mengine, jinsi katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia uhusiano wa Tanzania na nchi nyingine ulivyoimarika, aliweka wazi vipaumbele vya Serikali kwa mwaka 2024/2025.

Aidha, ameeleza jinsi Serikali ilivyo katika hatua za kukamilisha kutoa hadhi maalum kwa Dispora na jinsi Tanzania inavyohili ushindani kimataifa.

Wizara imeliomba Bunge kuidhinisha Sh241.069 bilioni ambapo kati ya fedha hizo sh. bilioni 229.4 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. bilioni 11.6 ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

Vipaumbele kwa mwaka 2024/2025

Akieleza vipaumbe vya Wizara, Waziri Makamba amesema Serikali imepanga kushamirisha kuliko ilivyowahi kutokea utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ili kuchochea Uwekezaji, Utalii, na Biashara pamoja na kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa maendeleo ya Nchi kwa Ujumla;

Vingine ni Kukuza ushirikiano wa kimkakati pamoja na kuhakikisha ushiriki wenye tija wa Tanzania katika jumuiya na mashirika ya kikanda na kimataifa ili kulinda maslahi mapana ya taifa; pamoja na kustawisha diplomasia ya kisasa na kujenga uhusiano wa karibu na nchi washirika;

“Tutaifanya Tanzania kuwa na ushawishi na kinara kwa nchi nyingine katika masuala mtambuka, kwenye Jumuiya na Mashirika ya Kikanda na Kimataifa ili Tanzania ikisema isikilizwe,” alisema Waziri Makamba na kuongeza;

“Kuongoza na kushiriki katika jitihada za kikanda na kimataifa za kudumisha amani, ulinzi na usalama ili kuhakikisha nchi yetu inabaki kuwa kioo cha amani na usalama.”

Kipaumbele kingine ni kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, kuimarisha utawala bora na rasilimaliwatu pamoja na kutekeleza miradi ya ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi, makazi ya watumishi na vitega uchumi katika balozi za Tanzania na makao.

Waziri Makamba amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara imepanga kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ili kuhakikisha inatoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Taifa na kutimiza azma Rais Samia.

Aidha, amesema Wizara imejipanga kuimarisha sauti ya Tanzania katika jumuiya ya Kimataifa ili kuimarisha zaidi hadhi na heshima ya nchi katika anga za kimataifa. Tutahakikisha tunapiga kura kimkakati na kuongozwa na Sera ya kutofungamana na upande wowote.

“Nchi yetu itaongeza ushiriki katika majukwaa yanayojadili masuala ya kidunia hususani masuala ya kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi na matumizi endelevu ya rasilimali,” anasema.

Anasema mwaka ujao wa fedha Wizara itaweka msisitizo mkubwa katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi na kuhakikisha uhusiano wetu na nchi nyingine na taasisi za kimataifa unaleta manufaa thabiti katika uchumi wa nchi yetu.

*** Uhusiano wa Tanzania na nchi zingine waimarika zaidi

Waziri Makamba, alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Uhusiano baina ya Tanzania na nchi nyingine umeimarika.

Amesema nchi yetu imejiongezea marafiki na kuimarisha urafiki uliokuwepo na nchi mbalimbali.

“Mafanikio haya yamewezeshwa na ziara zilizofanywa na viongozi wa kitaifa kwenye nchi mbalimbali. Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 Wizara iliratibu ziara 31 za Viongozi Wakuu wa Kitaifa nje ya nchi.

Aidha, Wizara iliratibu ziara 12 za kikazi za Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika mataifa mbalimbali,” alisema na kuongeza;

“Ziara za Viongozi wetu wa Kitaifa zimeliletea Taifa letu mafanikio makubwa ya kiuchumi.”

Mafanikio

Waziri makamba amesema ziara za viongozi nje ya nchi zimeleta baadhi ya mafanikio yafuata;

Moja, kuimarisha uhusiano wa nchi yetu na nchi marafiki zetu, na taasisi za kimataifa jambo ambalo linafungua milango ya kuongeza manufaa ya kiuchumi tunayoyapa kupitia uhusiano wetu.

Mbili, ni kusaini mikataba na makubaliano ya ushirikiano (MOUs) 78 katika sekta mbalimbali, tatu upatikanaji wa nafasi za masomo kwa Watanzania na nne ni upatikanaji wa fursa za ajira kwa Watanzania katika nchi mbalimbali.

Tano, amesema ni upatikanaji wa soko la mazao kwa wakulima wetu;
sita, upatikanaji wa fedha za miradi ya kimkakati kwa mfano reli ya kisasa (SGR) na Bandari ya Mangapwani, Zanzibar na saba kuvutia uwekezaji kiasi cha kufikia miradi yenye thamani ya dola bilioni 5.7 kwa mwaka 2023.

Nane, Makamba ni kuipa Tanzania fursa kuongoza mijadala ya kidunia yenye maslahi kwa nchi yetu, tisa kuvutia watalii kuja kutembelea Tanzania baada ya kupata taswira nzuri ya nchi yetu kupitia ziara za viongozi wetu na kumi wataalamu wa Tanzania kutoka Vyuo Vikuu na Taasisi nyingine kupata fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu na wenzao wa nchi mbalimbali kupitia makubaliano yanayowekwa kwenye ziara hizo.

Kicheko kwa diaspora

Kuhusu Diasipora, Waziri Makamba, amesema wana umuhimu mkubwa kutokana na mchango wao katika maendeleo ya Taifa. Alitoa mfano kwamba, mwaka 2023, Diaspora wa Tanzania walituma fedha nyumbani kiasi cha Dola za Marekani milioni 751.6.

“Kwa kuzingatia umuhimu wao, Serikali imejumuisha masuala ya Diaspora katika mapitio ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 na Sera Mpya ya Ardhi ya 2024 na kutoa Hadhi Maalum (Special Status) kwa Raia wa nchi nyingine Wenye Asili ya Tanzania ili kuwapa haki na upendeleo mahsusi,” alisema na kuongeza;

“Mwaka huu Serikali itakamilisha kutoa Hadhi Maalumu (Special Status) kwa Raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania (Tanzania Non- Citizen Diaspora). Katika kutekeleza hili, Serikali itawasilisha katika Bunge hili mwezi ujao muswada wa mabadiliko ya sheria utakaokuwa na marekebisho madogo ya Sheria za Uhamiaji Sura ya 54 na Sheria ya Ardhi Sura ya 113.”

Diplomasia ya uchumi kupewa msukumo mpya

Waziri Makamba alisema Msisitizo wa Sera yetu ya Mambo ya Nje ni Diplomasia ya Uchumi.

“Ninayo furaha kulifahamisha Bunge lako kuwa, Wizara imekamilisha rasimu ya awali ya Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

Mkakati huu umeianisha maeneo saba ya kipaumbele ambayo Wizara itayatilia mkazo katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi. Maeneo hayo ni pamoja na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, kuvutia watalii kuja Tanzania na kutafuta misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka nje.

Nyingine ni kutafuta fursa za ajira na masomo kwa Watanzania nje ya nchi, kujenga taswira nzuri ya nchi yetu kimataifa
(vii) ​Kujenga uwezo wa kitaasisi wa Wizara, na Wizara na Taasisi nyingine kusimamia vizuri utekelezaji wa Mkakati wa Diplomasia ya Uchumi.