January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ni bajeti yenye neema kwa Watanzania

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online Dar es Salaam

NI Bajeti ya viwango inayokwenda kulainisha na kupunguza makali ya maisha kwa wananchi wote. Hii inatokana na vipengele kadhaa vilivyoanishwa na serikali kupitia Mawaziri wa Kisekta na kujumuishwa na Wizara ya Fedha na Mipango, chini ya Waziri wake Mheshimiwa Mwigulu Nchemba.

Tanzania imejiwekea utaratibu wa kujadili na kuchanganua ndani ya Bunge ili kutengeneza bajeti bora kwa mustakabali wa nchi zao. Kwa Taifa kama Tanzania, nchi inayojipambanua na yenye shauku ya kukua kiuchumi, imejidhatiti kwa kubuni, kusimamia na kupitisha bajeti inayotoa ahueni kwa wananchi wake na kuongeza kazi ya ukuaji wa uchumi, ajira, na kipato.

Chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Watanzania wanakwenda kuyapata majibu ya matatizo yao kupitia hoja muhimu zilizowagusa.

Baadhi ya vipengele hivyo katika bajeti ya 2022/2023 ni sekta za uzalishaji za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Nishati, Uwekezaji na Biashara zinagusa na kutegemewa na watanzania walio wengi.

Kwa umuhimu wake, sekta hizi zilijadiliwa kwa kina na wabunge. Nzuri zaidi, serikali sikivu chini ya jemedari wake Mheshimiwa Samia, mengi kati ya yaliyojadiliwa katika Bunge hilo, yamechukuliwa na kufanyiwa kwa kazi kwa faida ya Watanzania wote.

Serikali inahakikisha kuwa mikopo ya ndani na nje inayochangia ukuaji wa deni la Taifa ambalo hata hivyo baado ni himilivu inakwenda kwenye miradi ya maendeleo moja kwa moja ili kupunguza makali ya maisha. Hata ulipaji wake si mgumu kwa sababu ni mzunguuko wa kawaida ndani ya serikali.

Kwa vyovyote iwavyo, deni hilo ni ishara ya uwapo wa jitihada za kuleta maendeleo kwa Taifa kwa sababu fedha hizo zinaenda kwenye ujenzi wa miradi ya kimkakati kama barabara, madaraja, miradi ya umeme, reli nk.

Bajeti inaonyesha inaenda kupunguza makali ya maisha na kuchochea uchumi, ajira, kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, uwekezaji na biashara. Serikali imeamua kujikita humo kwa lengo la kutatua changamoto zilizochangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha uchumi wa Taifa.

Katika suala la miundombinu na huduma za kijamii kama elimu, afya, maji na kuinua kaya maskini kwa kupitia Mfuko wa kuendeleza kaya masikini kwa kupitia TASAF nayo ni kati ya mambo yenye tija yaliyozingatiwa kama chanzo cha kuongeza kasi ya ufufuaji na uimarishaji wa sekta ya uzalishaji kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania.

Serikali imeamua kujitwisha mzigo wa kutoa ruzuku kwenye huduma za kimkakati kama vile mafuta ya kula, ngano, mbolea na mafuta ya nishati (petrol). Kipengele muhimu kama hiki huwa kinazalisha mfumko wa bei na kuongeza makali ya maisha kwa wananchi.

Ni mara kadhaa nchi imeingia kwenye uhaba wa mafuta ya kula. Imeshatokea pia mafuta kupanda bei mara dufu kiasi cha kupandisha nauli kwenye vyombo vya usafiri. Kwa kupitia bajeti ya 2022/2023 ambayo serikali imetenga Sh Bilioni 100 kwa mwezi kama njia ya kupunguza mfumko wa bei ya mafuta ya nishati nchini Tanzania.

Sasa wakulima wa korosho, mtama, mahindi, chai na wote katika nchi hii, watafanya kazi ya kuzalisha mazao yao pasi na changamoto kama zile zilizozoeleka.

Katika hili, serikali kupitia wizara yake ya Fedha imeamua kwa dhati kupunguza makali ya maisha kwa vitendo sanjari na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. Sekta za kipaumbele zinazogusa idadi kubwa ya watu kama kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na biashara zimefanyiwa kazi na kupatikana ufumbuzi kwa kiasi kikubwa.

Wakati anahitimisha bajeti yake bungeni mjini Dodoma, Waziri Nchemba alisema ni matumaini yao kuwa nchi itasonga mbele kwa kutatua kero nyingi na kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata ahueni katika maisha yao kwa namna moja ama nyingine

“Serikali inalenga kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya milioni tatu katika sekta ya kilimo ifikapo mwaka 2025. Hii itafanyika kwa kuongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 8,500,000, sawa na asilimia 50 ya eneo lote linalolimwa nchini ifikapo 2030,” Alisema Waziri Nchemba.

Aidha imeongeza pia uboreshaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji, miundombinu bila kusahau mkazo uliowekwa kwenye mradi wa kuhudumia kaya masikini chini ya mfuko wa TASAF.

Ilichofanya serikali ni kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa fedha kwenye vyanzo vyake pamoja na kuipanua bajeti yake kadri iwezavyo. Kwa mfano, serikali ilitenga bajeti Shilingi Trilioni 34.88 kwa mwaka 2020/2021.

Mwaka wa bajeti 2021/202 ilitenga Shilingi Trilioni 36.3. Kama hivyo haitoshi, mwaka wa 2022/2023 imeweka bajeti ya Shilingi Trilioni 41.48 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Shilingi Trilioni 5.

Haya ni mapinduzi makubwa katika bajeti ya nchi yetu. Walau dhamira njema inaonekana. Ikumbukwe kuwa ni Trilioni 2 tu zilizoongezwa katika bejeti ya 2021/2022 kutoka kwenye kiwango cha Shilingi 34.88 kutoka kwenye bajeti ya 2020/2021.

Katika mwaka huu 2022/2023 mapato ya ndani ni asilimia 68, wakati mikopo ya nje na ndani ikiwa ni asilimia 21, huku fedha za misaada zikitarajiwa kuwa kwa asilimia 11 tu.

Hii inaonyesha kuwa serikali imewekeza zaidi katika ukusanyaji wa mapato yake kutoka kwenye vyanzo vya ndani. Na kwenye zile fedha za mikopo zitakazopatikana, zitaenda moja kwa moja kwenye ujenzi wa miundombinu, madarasa, vituo vya afya ili kupunguza kama sio kuondoa kabisa uzoroteshaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Miradi itasaidia kufungua uchumi na kuongeza kipato kwa nchi ambacho asilimia ndogo inalipa deni huku faida kubwa ikienda kwa wananchi kutokana na kasi ya maendeleo.

Serikali haikopi kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ila kutumia mikopo hiyo kujenga miradi ya maendeleo. Katika hoja za baadhi ya watu kuwa serikali ina mpango wa kuileta upya kodi ya kichwa ni upotoshaji na ukosefu wa uelewa.

Kinachofanyika ni uboreshaji na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili nchi iweze kujiendesha kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani.

Mapato hayawezi kuongezeka endapo mkakati madhubuti hautawekwa wa kuwajua na kuwaelimisha wale wanaostahili katika suala zima wa ulipaji wa kodi. Serikali haifanyi biashara. Kazi yake ni kuweka mazingira rafiki ya ulipaji wa kodi.

Kilichofanyika ni kuibua mchakato wa usajli wa wenye umri wa kulipa kodi na sio kuwa na mpango wa kutoza kodi ya kichwa kama baadhi yao wanavyojaribu kupotosha.

Kodi itakusanywa kwa kuzingatia kipato kutoka kwa wale waliotambuliwa na aina ya biashara wanazofanya. Wale wenye vipato vikubwa nao watatozwa kodi kulingana na sheria zilizopo. Hili likifanyika kwa ukamilifu, litaongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi kwa kiwango cha juu.

Kazi ya serikali itasaidia kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kufanya makadirio ya kodi kwa wafanyabiashara wadogo ambao hawana uwezo wa kutunza kumbukumbu na kutengeneza hesabu za biashara zao.

Kwa kuliangalia hilo, utagundua kuwa serikali inajibu maswali yote kutokana na uwapo wa bajeti bora na shirikishi kwa viongozi wa wizara na wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi wao.
Watanzania.