June 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ni bajeti ya ukombozi

*Ni ya trilioni 49. 35 inaenda kuwezesha Watanzania kuwa na maisha bora chini ya uongozi wa Rais Samia, itachochea ukuaji uchumi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI wa Fedha, Mwigulu Nchemba, amewasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2024/2025 ya sh. trilioni 49. 35 ambayo inalenga kuwezesha Watanzania kuwa maisha bora.

Aidha, Waziri Nchemba ameainisha maeneo mbalimbali ambayo Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuyaboresha ili kuwawezesha Watanzania kuwa na maisha bora.

Waziri Nchemba amewasilisha bajeti hiyo Bungeni jijini Dodoma, Juni 13, mwaka huu ambapo ametaja maeneo ambayo Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia itaendelea kuyaboresha.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni ya miundombinu ya nishati, usafiri na usafirishaji; kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kupitia sera madhubuti ili kuwezesha ushindani huria wa sekta binafsi, kuboresha mifumo ya elimu na mafunzo; na kuunganisha tafiti na maendeleo na shughuli za kiuchumi zenye tija.

“Bajeti ya mwaka 2024/25 inalenga kuwawezesha Watanzania kuwa na maisha bora kwa kuendeleza juhudi za kujenga msingi wa uchumi wa viwanda ili kupanua fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi endelevu wa jamii,” alisema Waziri Dkt. Nchemba.

Amefafanua kwamba Bajeti ya mwaka 2024/25 inalenga kuendeleza juhudi za kujenga msingi wa uchumi wa viwanda ili kupanua fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi endelevu wa jamii.

” Ili kufikia matamanio haya, rai yangu kwa Watanzania wenzangu, na hasa sisi viongozi ni lazima tujitoe kuijenga Tanzania kwa kumuunga mkono Rais wetu kwa vitendo.

Hivyo, ni lazima tufanye kazi kwa bidii tukijielekeza kutekeleza malengo tuliyojiwekea ya kujenga uchumi imara unaotengeneza ajira ili kila mtanzania anufaike na matunda ya jasho lake.

Kuhusu uchaguzi, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kugharamia mchakato mzima wa chaguzi hizo.

“Nitoe rai kwa viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa tunatumia haki yetu ya kikatiba kuchagua au kuchaguliwa kwa amani, undugu na upendo.

Aidha, tuhakikishe kuwa viongozi tunaowachagua wawe ni waadilifu, wasikivu, wazalendo, wachapa kazi na wanaotoka ndani ya chama cha siasa kinachotetea maslahi na haki za wanyonge na chama hicho ni Chama Cha Mapinduzi.

Kuhusu sura ya bajeti, Waziri Dkt. Mwigulu alisema kwa mwaka 2024/25, Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya sh. trilioni 49.35, sawa na ongezeko la asilimia 11.2 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24.

“Ongezeko la bajeti kwa kiasi kikubwa limetokana na kugharamia: deni la Serikali ambalo limeongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi, kuongezeka kwa viwango vya riba na kuiva kwa mikopo ya zamani; ajira mpya; ulipaji wa hati za madai,” alisema na kuongeza;

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025; na maandalizi ya michuano ya mpira wa miguu ya mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ikiwemo ujenzi na ukarabati wa viwanja.

*** Mapato

Amesema mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa jumla ya sh.trilioni 34.61, sawa na asilimia 70.1 ya bajeti yote na asilimia 15.7 ya Pato la Taifa.

“Kati ya mapato hayo, mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanakadiriwa kuwa sh. trilioni 29.41, mapato yasiyo ya kodi yatakayokusanywa na Wizara, Taasisi na Idara zinazojitegemea sh. trilioni 3.84 na mapato yatakayokusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa sh. trilioni 1.36,” alisema.

Amesema misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo inakadiriwa kuwa shilingi trilioni 5.13.

“Ni matarajio yetu kuwa rasilimali zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa zitatolewa kwa wakati na kwa kiasi kilichoahidiwa. Nasi, kwa upande wa Serikali tunaahidi kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizo kama ilivyokusudiwa,” alisema.

***Mkopo

Ameongeza kwamba Serikali inakadiria kukopa sh. trilioni 6.62 kutoka soko la ndani ambapo sh. trilioni 4.02 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na sh. trilioni 2.60 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Aidha, amesema Serikali inakadiria kukopa sh. trilioni 2.99 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Amesema ili kuhakikisha soko la mitaji la ndani linaendelea kuwa chanzo muhimu cha fedha, Serikali itaendelea kutoa hati fungani kizio (benchmark bonds) kwa lengo la kujenga viwango vya bei rejea na shindani katika soko la fedha na mitaji nchini.

Aidha, alisema Serikali itaendelea kufungua wigo kwa wawekezaji kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

***Matumizi

Waziri Dkt. Mwigulu alisema katika mwaka 2024/25, Serikali imepanga kutumia jumla ya sh. trilioni 49.35.

Alisema Kiasi hicho kinajumuisha sh.trilioni 15.74 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu; sh. trilioni 11.77 kwa ajili ya mishahara ikiwemo ajira mpya pamoja na upandishaji wa madaraja kwa watumishi; sh. trilioni 2.17 kwa ajili ya mifuko ya reli, barabara, maji, REA na TARURA; na ruzuku ya maendeleo ya sh. trilioni 1.19 kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati pamoja na Programu ya Elimumsingi na Sekondari bila Ada.