January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NHIF yarejesha Toto Afya Kadi ,yazindua vifurushi vipya

Na Joyce Kasiki:-Timesmajira online ,Dodoma

SERIKALI imerejesha huduma ya matibabu kwa watoto ‘ Afya toto kadi’ huku ikizindua Mifumo ya upatikanaji huduma za Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kwa wananchi bila kufika ofisi za NHIF.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mifumo hiyo,Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema suala la kuondolewa kwa Toto afya kadi lilikuwa ni kilio cha watu wengi kwani mpango huo ulisaidia sana familia za wananchi wengi hasa zile zilizokuwa na changamoto za kiafya.

Hata hivyo amesema ,pamoja na uzuri wake lakini ulileta hasara kwa kuwa Kila shilingi 100 mtoto alitumia takriban shilingi 600.

Mhagama amesema kuwa mpango wa sasa wa usajili wa Toto Afya Kadi utafanyika kwa mtoto mmoja mmoja iwapo itatokea mtoto husika hayupo shule, hii ni hatua kubwa na yakujivunia katika sekta nzima ya afya.

Pia Serikali imezindua kifurushi cha Ngorongoro chenye huduma 445 na Serengeti chenye huduma 1,815 ambavyo vyote vimelenga kuhudumia watanzania katika eneo la sekta ya Afya.

“Mara baada ya uzinduzi wa vifurushi hivi, ajenda iliyopo mbele ni ubora wa huduma,hivyo watoa huduma mnapaswa kuibeba ajenda hii na kutoa huduma zenye tija kwa maslahi ya umma wa watanzania ili waone umuhimu wa Bima na ifikapo 2030 Tanzania iwe imetimiza malengo ya kidunia.”amesema na kuongezea kuwa

” Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa Vifaa Tiba na Dawa ambapo kwa sasa upatikanaji wa dawa ni wastani wa asilimia 86 ambayo imewezesha wananchi kunufaika na huduma hizo ambapo
takriban vituo 9,826 nchi nzima, kati ya vituo hivyo, vituo 7,366 (sawa na 75%) ni vya Serikali, vituo 1,375 (sawa na 14%) vinamilikiwa na watu binafsi,

“Vituo 1,006 (sawa na10.2%) vinavyomilikiwa na mashirika ya dini na vituo 79 (sawa na 0.8%) vinamilikiwa na mashirika ya Umma. Vilevile kuna jumla ya kliniki 987 na Maabara 1,590”,

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI Elibariki Kingu ameishukuru Serikali kwa kutekeleza maagizo ya Bunge huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kulisemea suala la Bima ya Afya.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka amesema kuzinduliwa kwa mfumo wa kidijitali kumewawezesha kushughulikia folio 1,200 kwa dakika 45 tofauti na awali ambapo walishighulikia folio 800 tu kwa siku.