July 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NHIF yaingia mkataba wa mashirikiano na ZHSF

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) wameingia mkataba wa  mashirikiano ya Huduma za Afya kwa wanachama wa ZHSF kupata huduma Tanzania Bara.

Lengo likiwa ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya za uhakika na endelevu kwa wananchi na wakazi wote wa Zanzibar bila kuwa na kikwazo cha fedha pale wanapozihitaji .

Makubaliano hayo ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha katika kugharamia huduma za afya.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Juni 28,2024 Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bernard Konga na Yassin Juma Mkurugenzi Mkuu wa mfumo wa wa Huduma za Afya Zanzibar ZHSF,Konga amesema kuwa makubaliano hayo ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha katika kugharamia huduma za afya.

“Mwaka 2023 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ilianzisha Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) kwa  kuhakikisha kuwa ZHSF inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar Na. 1/2023.

“Kutambua uzoefu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), katika uendeshaji wa mfumo wa bima ya afya nchini, Julai Mosi, 2024 ZHSF itaanza rasmi majukumu yake kwa kuhudumia wanachama na wategemezi wake kupitia Vituo vya kutolea huduma vilivyosajiliwa na NHIF Tanzania Bara, ” Amesema

Hivyo Konga amesema katika kufanikisha huduma kwa wanachama hao, NHIF na ZHSF zimesaini mkataba wa makubaliano wa mashirikiano katika utoaji wa huduma kwa
wanachama wake.

Amesema hatua hiyo inatokana na uzoefu, wigo mpana wa vituo vya kutolea huduma vilivyosajiliwa na NHIF nchi nzima.

Ameeleza Maandalizi yaliyofanywa na NHIF kwa upande wa NHIF, hatua mbalimbali za maandalizi na utayari wa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mashirikiano zimefanyika ili kuhakikisha wanachama hao wanapata huduma bila ya changamoto yoyote.

Aidha amesema Ofisi zote za NHIF zilizoko katika Mikoa yote ziko tayari na
zimejipanga kutoa huduma na kutoa msaada utakapohitajika, Mifumo ya utambuzi imeimarishwa zaidi ili kurahisisha utambuzi wa wanachama wanapofika katika vituo vya kutolea huduma, Kufanya malipo kwa watoa huduma kwa wakati pindi
wanachama hawa watakapopata huduma za matibabu katika vituo husika,  Kuandaa Ofisi kwa aiili watumishi wa ZHSF watakaokuwa wanahudumia wanachama kwa upande wa Tanzania Bara.

Amesema Utaratibu utakaotumika kwa wanachama wa ZHSF kupata huduma za matibabu, Wanachama wa ZHSF watapata huduma kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya tiba nchini kama inayotumika kwa wanachama wa NHIF. Taratibu hizo ni pamoja naWanachama na wategemezi wa ZHSF watatumia kadi ya uanachama ya ZHSF badala ya kadi ya NHIF.

Vituo vitatumia Mifumo ya utambuzi inayotumiwa na NHIF
katika kuhakiki uhalali wa wanufaika;
Kutumia mfumo wa rufaa katika kupata huduma ambapo
mwanachama anaweza kuanzia ngazi ya hospitali ya wilaya ama ngazi ya
chini kupata huduma husika.

Ushughulikiaji wa Changamoto za Kihuduma Katika kuhakikisha wanachama wanapata huduma wanazohitaji, ZHSF na NHIF zimejipanga kwa kuweka Maofisa Maalum kutoka ZHSF ambao watakuwa katika Ofisi za NHIF kwa ajili ya kushughulia changamoto zinazojitokeza hususan za kihuduma.

Aidha kwa sasa Hospitali nyingi za NHIF zinayo madawati maalum ya Watum1shi wake ambao moja ya majukumu yao ni kutoa usaidizi kwa wanachama wanaokwama ama kukutana na changamoto katika kupata huduma za matibabu.

Mfuko unawahakikishia wanachama wake upatikanaji wa huduma bora Za
matibabu katika vituo vyote wa kutolea huduma vilivyosajiliwa na MYuko.

Akizungumka katika kikao hicho  Mkurugenzi Mkuu wa mfumo wa Huduma za Afya Zanzibar ZHSF,Yassin Juma amesema Kuanzia mwezi wa Julai, 2024 watumishi ambao walikuwepo NHIF kutoka sekta ya umma watarudi rasmi ZHSF na wafanyakazi wote waliopo sekta binafsi wataanza kupata huduma ZHSF kuanzia tarehe 1 Septemba Mosi, 2024.

Vilevile ZHSF itafungua ofisi Tanzania Bara ili kuratibu kwa ukaribu maswala yote ya huduma.

Amesema Mwezi wa Machi, 2024 ZHSF ilianza usajili wa sekta Binafsi na huku tukiandaa mikakati ya kuelekea katika usajili wa sekta isiyo rasmi na makundi mengine yasiyokuwa na uwezo kama ilivyoelekezwa katika Kifungu cha 2 cha Sheria ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar Nam.1 ya 2023.

“Katika kipindi cha mpito cha kuwafikia wanachama wetu walioko Tanzania Bara, tulishirikiana na wenzetu wa NHIF ili kuweka utaratibu wa muda wa kuwawezesha wanachama hao kupata huduma za afya, ambapo ZHSF ilikua ikilipa michango ya wanachama hao NHIF,” amesema.

Na kuongeza “Vilevile, ZHSF na NHIF zilikua zikishirikiana kwa wanachama wote ambao kabla ya kuanzishwa kwa ZHSF walikua ni wanachama wa NHIF ambapo hadi sasa NHIF inaendelea kuwapatia huduma wanachama hao kwa kutumia kadi za NHIF, “

Hata hivyo amebainisha kuwa Kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha Sheria Nam.1 ya 2023, Mfuko umepewa uwezo wa kuwafikishia wanachama wake huduma za afya nje ya Zanzibar, ambapo kwa kuanzia ZHSF imeanza kuwafikia wanachama wake walioko Tanzania Bara.