Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa – NHC kutumia teknolojia ya kisasa ili kuweza kuongeza nyumba za makazi ambazo zitasaidia kupunguza pengo la mahitaji ya nyumba nchini.
Waziri Dkt. Mabula ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea mradi wa nyumba za makazi mia tano na sitini wa Samia Housing Scheme – SSH unaotekelezwa na NHC katika eneo la Tanganyika Packers Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa ulimwengu wa sasa umejikita katika teknolojia hivyo ili kuweza kuleta maendeleo yoyote teknolojia inapaswa kutumika kikamilifu. Ni wakati muafaka sasa na NHC kuweza kutumia teknolojia ambayo itasaidia kuongeza nyumba za makazi nchini.
“Tanzania ina uhaba wa nyumba milioni tatu na laki nane na kwamba kwa kasi tunayoenda nayo ya kujenga nyumba kwa mfumo tulio nao kwa sasa ninyi NHC na watu wengine hatutaweza kutatua tatizo la makazi hapa nchini,” amesema Dkt. Mabula
Alibainisha kusema kuwa ili kuweza kupata nyumba nyingi za makazi umefika wakati sasa wa kuanza kutumia teknolojia ili kuweza kusaidia upatikanaji wa nyumba nyingi za makazi nchini.
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka vibarua wanaofanya kazi katika mradi huo kuwa waaminifu na kujiepusha na vitendo viovu ukiwamo wizi wa vifaa kwani kwa kufanya hivyo kutasababisha wao kukosa uaminifu na hivyo kukosa kazi.
Amesisitiza kuwa uaminifu ni nyenzo muhimu ambayo kila mtu anayehusika na utekelezaji wa mradi huo anapaswa kuwa nayo ili kuweza kutimiza malengo ya mtu binafsi, lakini pia malengo ya Shirika ambayo yanatarajia mradi huo ukamilike kwa wakati katika ubora na kwa viwango vya hali ya juu.
“Tutekeleze mradi huo kwa uaminifu mkubwa kwani Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliridhia NHC kupata shilingi Bilioni mia moja sabini na sita kwa ajili ya kuiamsha miradi iliyokuwa imelala na kuianzisha mingine mipya, na kuongeza kuwa mradi huo ni mpya na Serikali isingependa kusikia kelele zozote juu ya utekelezaji wake,” amesema Dkt. Mabula.
More Stories
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo