November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ngwelo wanufaika miradi ya barabara, maji, umeme, kituo cha afya

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Lushoto

MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu Bosnia, amesema haijawahi kutokea Kata ya Ngwelo kupata miradi mikubwa tangu nchi kupata Uhuru, kwani kwa sasa kata hiyo ina mradi wa barabara, maji, umeme na Kiruo cha Afya Ngwelo.

Na Shekilindi amempongeza Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha kwa ajili ya miradi hiyo ikiwemo ya ujenzi wa bweni la wasichana Shule ya Sekondari Ngwelo, na Zahanati ya Kijiji cha Kigulunde, na ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi na sekondari.

Shekilindi aliyasema hayo Machi 3, 2023 alipofanya ziara kwenye Kata ya Ngwelo, ambapo pamoja na mambo mengine, alikagua ujenzi wa Zahanati ya Kigulunde ambayo imeanza kutoa huduma, ujenzi wa Kituo cha Afya Ngwelo, na sehemu itakapojengwa bweni la wasichana Shule ya Sekondari Ngwelo.

“Wananchi naomba mumuombee sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani haijawahi kutokea tangu Uhuru kupata miradi mikubwa kama hii iliyogharimu mabilioni ya fedha. Mama ameleta mradi mkubwa wa barabara kiwango cha changarawe ambao unasimamiwa na TARURA. Mradi huo ni wa sh. bilioni 3.5, na unajenga barabara ya kilomita 72 ikipita hapa kutokea Mlalo- Ngwelo- Mlola, Makanya, Milingano hadi Mashewa. Na bado, kuna kilomita tano za barabara ya lami zinakuja.

“Mama ameleta mradi wa maji wa sh. milioni 500 ukisimamiwa na RUWASA, na mradi huo umekamilika. Ameleta sh. milioni 250 kwa ajili ya Kituo cha Afya Ngwelo, na baadhi ya majengo yamekamilika. Na ataleta sh. milioni 250 nyingine ili kukamilisha majengo yaliyobaki. Pia ameleta sh. milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana Sekondari ya Ngwelo, achilia mbali ujenzi wa vyumba vya madarasa msingi na sekondari. Pia kwa mara ya kwanza, Ngwelo tumepata umeme” alisema Shekilindi.

Shekilindi alisema hata Mfuko wa Jimbo umetoa fedha nyingi kwenye Kata ya Ngwelo kuliko kata zote za jimbo hilo. Kwani wamepata sh. milioni 10, ambapo sh. milioni saba zimetumika kununua kiwanja kunapojengwa bweni la wasichana Shule ya Sekondari Ngwelo, sh. milioni mbili kusaidia kutengeneza uwanja wa michezo, na sh. milioni moja kuongeza nguvu ujenzi wa choo Zahanati ya Kigulunde.

Hata hivyo, Shekilindi alitahadharisha wananchi kuwa kama wataendelea kuharibu mazingira ikiwemo vyanzo vya maji, Mradi wa Maji Ngwelo utashindwa kuwa endelevu, kwani hata kabla mradi huo haujakabidhiwa rasmi kwa wananchi, tayari chanzo cha maji kimepungua, huku baadhi ya wananchi wakikata kwa makusudi mabomba yanayotoa maji kwenye tenki kwenda kwa wenyeji.

“Kuna watu wanakata mabomba kabla mradi haujakabidhiwa rasmi. Mama Samia ametoa sh. milioni 500, hivyo mradi huu ni wa fedha nyingi, na najivuna kwa mradi huu, na mimi kutembea kifua mbele, lakini leo hii kuna watu wanaharibu miundombinu ya maji kwa kukata mabomba. Wananchi toeni taarifa kwa Ofisa Mtendaji Kata ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa watu hao” alisema Shekilindi.

Mwananchi Sadick Kijangwa aliomba gharama za kuingiza maji majumbani zipungue, kwani ada ya sh. 40,000 kwa ajili ya kuingiziwa maji nyumbani ni kubwa, hasa ukichukulia hadi mwananchi kuingiza maji ndani ya nyumba, gharama yake ni zaidi ya sh. 200,000.

Akijibu baadhi ya hoja kutoka kwa wananchi, Mwakilishi wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto, Charles Ligola, alisema Mradi wa Maji Ngwelo ni wa sh. milioni 500, na umejengwa matenki mawili yenye ujazo wa lita 90,000 kila moja. Tenki moja linahudumia Kijiji cha Kihitu na jingine Kigulunde.

“Lakini baadhi ya maeneo wananchi wamekosa maji hasa Kigulunde sababu wananchi wanakata mabomba kwa makusudi kiasi bomba haliwezi kufunguliwa kutoka kwenye tenki sababu maji yatapotea njiani. Chanzo cha maji cha kutosha hakuna. Mradi ni mkubwa, Tenki moja linajaa kwa siku tatu, hivyo inabidi tutoe maji kwa mgao

“Kuna uharibifu mkubwa, na kuna watu wanalima kwenye chanzo. Hivyo hata hayo maji machache muda si mrefu hayatapatikana. Hivyo mheshimiwa Mbunge, mradi wa maji haujazinduliwa, lakini tayari kuna changamoto. Hata hivyo, tumekuja na suluhisho, tutachimba visima ambavyo vitasaidia kupandisha maji kwenye matenki hayo. Na hapa Ngwelo tumeshaunda Bodi ya Maji, na jengo lao lipo hatua ya mwisho kukamilika” alisema Ligola.

Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi ‘Bosnia’ (katikati) akikagua shimo la choo Zahanati ya Kijiji cha Kigulunde, Kata ya Ngwelo. (Picha na Yusuph Mussa)
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi ‘Bosnia’ akizungumza na wananchi kwenye Zahanati ya Kijiji cha Kigulunde, Kata ya Ngwelo. (Picha na Yusuph Mussa).
Jengo la Mama na mtoto Kituo cha Afya Ngwelo. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi ‘Bosnia’ (katikati) akikagua jengo la Mama na mtoto, Kituo cha Afya Ngwelo. Kulia ni Diwani wa Kata ya Ngwelo Yosse Shekaholwe na kushoto ni Mganga Mfawidhi Jamillah Msengi. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi ‘Bosnia’ (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ngwelo Jamillah Msengi (kushoto). (Picha na Yusuph Mussa).
Moja ya vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu Shule ya Sekondari Ngwelo vilivyojengwa kwa fedha za EP4R kutoka Serikali Kuu. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi ‘Bosnia’ (kulia), akikagua maabara ya vyumba viwili inayojengwa Shule ya Sekondari Ngwelo. Maabara hiyo ina zaidi ya miaka kumi haijakamilika. (Picha na Yusuph Mussa).