March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NFRA yawahimiza wananchi kuhifadhi chakula kwa Usalama ,yatoa Elimu kaika maonyesho ya 49 ya Biashara

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online

Pichani ni mfano wa magjhala ya kuhifadhia chakula

WAKALA  wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umewataka wananchi, wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya kupata elimu kuhusu uhifadhi salama wa chakula, sambamba na kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Hayo yamesemwa na Afisa Masoko wa NFRA, Bi. Eva Michael, alipokuwa akizungumza katika Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam, ambapo wakala huo umeweka banda maalum kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli zake na umuhimu wa kuhifadhi chakula kwa usalama.

“Tupo hapa kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi kuhusu uhifadhi bora wa chakula, lakini pia kuelezea kwa kina majukumu ya NFRA. Tunawakaribisha wakulima, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuja kutufahamu zaidi na kuona namna wanavyoweza kushiriki katika mnyororo wa hifadhi ya chakula,” alisema Bi. Eva.

Kuhusu majukumu ya Wakalanhuo Eva amesema, mojawapo ya majukumu makuu ya NFRA ni kununua, kuhifadhi na kuuza nafaka kwa lengo la kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya chakula ya kutosha kukabiliana na majanga au upungufu wa chakula.

Alibainisha kuwa hivi sasa NFRA ipo katika maandalizi ya awali ya msimu wa ununuzi wa nafaka mpya, ambapo wananchi na wakulima wanahimizwa kujiandaa kushiriki katika zoezi hilo muhimu.

Aidha amesema kwa sasa, maghala ya NFRA yana shehena ya kutosha ya nafaka mbalimbali ikiwemo mahindi, mpunga, mtama mweupe, mbaazi na dengu, ambazo zinaendelea kuuzwa kwa wadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya misaada, sekta binafsi na taasisi za umma.

“Tunawahakikishia wadau wetu wote kuwa chakula tulichonacho ni salama na kimehifadhiwa kwa kuzingatia viwango bora vya kitaifa na kimataifa.naendelea na mauzo kwa taasisi na wafanyabiashara mbalimbali, na tunakaribisha wale wanaotaka kuuza au kununua nafaka kupitia NFRA,” ameongeza Eva.

Aidha amesema,katika kufanikisha dhamira ya Taifa ya kuwa na akiba ya chakula ya uhakika na uhifadhi endelevu amesema, NFRA imeweka mkazo katika ushirikiano wa karibu na wananchi, ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya uhifadhi wa chakula majumbani, maghalani na katika mnyororo mzima wa usambazaji.

Kwa ujumla, ushiriki wa NFRA katika Maonyesho ya 49 ya Biashara unaendelea kuwa jukwaa muhimu la mawasiliano kati ya wakala na wananchi, na unalenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa uhifadhi bora wa chakula kwa maendeleo ya Taifa.