November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nesi akutwa na zigo la Heroin, Watuhumiwa sita wafikishwa mahakamani

Na Iddy Lugendo, TimesMajira Online

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata jumla ya kilogramu 877.217 za dawa za kulevya na kuzuia uingizaji wa kilogramu 122,047.085 na Lita 85 za kemikali bashirifu Nchini.

Dawa za hizo ni heroin kilogramu 174.112 zilizowahusisha watuhumiwa wawili na bangi kilogramu 703.105 zilizowahusisha watuhumiwa sita ambao wote wamefikishwa mahakamani.

Ameyasema hayo leo Juni 3,2022, Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za Kulevya nchini , Kamishna Jenerali Gerald Kusaya wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam

Amesema Mei 12,20022 katika eneo la Tabata relini wilaya ya Ilala, mkoa wa Dar es Salaam walikamata Kilogram 174.77 za dawa ya kulevya aina ya heroin. Katika tukio hilo Salum Shabani Mpangula (54), kabila mngindo, dini muislamu, mkazi wa mtaa wa reli – Tabata ambaye ni Nesi msaidizi Karikoo Dispensary amekamatwa kwa tuhuma za kusafirisha dawa hizo.

“Kufuatia upekuzi uliofanyika nyumbani kwa mtuhumiwa, paketi 162 zenye unga uliodhaniwa kuwa dawa za kulevya zilikutwa ndani ya viroba sita vilivyouwa vimehifadhiwa chumbani kwa mtuhumiwa, na paketi moja ya unga huo ilikuwa imewekwa kwenye mfuko mweusi wa nailoni na kufichwa chini ya kitanda”. Amesema Kamishna Jenerali Kusaya.

Pia amesema kuwa taarifa ya uchunguzi wa kitaalam kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa paketi zote 163 zilikuwa na dawa za kulevya aina ya heroin ambazo jumla yake ni Kilogramu 174.77. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Aidha, amesema Mamlaka imeteketeza jumla ya hekari 21 za mashamba ya bangi mkoani Arusha na jumla ya kilogramu 250.7 za dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine ambazo mashauri yake yalimalizika mahakamani, katika kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara.

Hivyo amesema katika kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi juu ya tatizo la dawa za kulevya; Mamlaka imeandaa muongozo utakaotumika kutoa elimu, imeshiriki kuandaa ujumbe juu ya tatizo la dawa za kulevya katika Mbio za Mwenge wa Uhuru zinazoendelea na kutoa elimu kwa Kamati za Ulinzi na Usalama, kamati za Afya na watendaji wa Serikali za Mitaa ili wasaidie kuongeza uelewa wa tatizo la dawa za kulevya kwa jamii.