November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NEMC yahimiza matumizi salama ya zebaki kulinda afya ya mazingira

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetaka wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kutumia njia mbadala ya uchenjuaji na kuacha matumizi hatarishi ya kemikali ya zebaki ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu na Mazingira.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira NEMC,Dkt.Menan Jangu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na athari za matumizi ya zebaki kwa afya ya binadamu na mazingira katika mkutano uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Baraza jijini Dar es Salaam.

Dkt.Menan amesema takribani zaidi ya watu milioni 1.5 nchini wanajishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini ambao wengi wao wanatumia kemikali ya zebaki ambayo ni rahisi na bei nafuu  katika shughuli za uchenjuaji madini lakini ina madhara makubwa kwa kusababisha magonjwa kama kansa, utindio wa ubongo na matatizo katika mfumo wa uzazi wa binadamu.

“Takribani zaidi ya watu milioni 1.5 wanajishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini ambao wengi wao wanatumia kemikali ya zebaki ambayo ni rahisi kuitumia lakini ina madhara makubwa kwa afya ya binadamu kama kansa, kuharibu mfumo wa uzazi na kusababisha ugonjwa wa utindio wa ubongo, ndiyo maana Baraza limejikita katika  utoaji wa  elimu kwa watumiaji hao kuacha kuitumia au endapo itatumiwa wavae vifaa vya kujikinga na kemikali hiyo ambayo ni hatarishi kwao na Mazingira,”amesema Dkt. Menan.

Pamoja na hayo Dkt. Menan ameongezea kuwa Baraza kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na Mfuko wa GF wanaendelea kutoa elimu juu ya athari za matumizi ya zebaki na linasisitiza shughuli zote za madini zifanyike katika utaratibu ambao hautakuwa hatarishi kwa jamii na mazingira.

Naye Mratibu Mkuu wa Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya zebaki (EHPMP) Mhandisi Dkt. Befrina Igulu ameongezea kwa kusema Baraza linaitaka jamii ichukue tahadhari ya matumizi ya zebaki ambayo ni hatari na endapo itatumiwa itumike kwa utaratibu maalumu, Pia ametoa wito kwa wamiliki wa mialo kuwa na vifaa kinga kwa wachenjuaji ili waweze kujikinga na kemikali ya zebaki na kusaidia  kupunguza athari kwa mifumo ya ikolojia, afya ya jamii na Mazingira.