Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limewataka akinamama wa Mkoa wa Dar es Salaam kutumia fursa za kibiashara zinazopatikana katika Mkoa huo ili kuanzisha shughuli za ujasiriamali na biashara ili kuleta matokeo chanya kwenye Familia zao na Taifa kwa ujumla kupitia programu ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati wa uzinduzi wa Programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA) katika Mkoa huo.
Amesema Rais Samia amekuja na programu hiyo ili kumuwezesha mwanamke wa nchini kutoka kwenye lindi la umasikini na anaendelea kushughulikia na mikopo ya wanawake na watu kwenye makundi maalum ili iende kwa walengwa.
“Juhudi za kila siku za shughuli za kijasiriamali ndio zitakazotutoa kimaisha na kuendelea kuchangamkia fursa za kiuchumi,” amesisitiza.
“Tunampongeza Rais Samia kwa kutuletea program hii Imarisha Uchumi na Mama Samia katika mkoa wetu, na sisi tumeipokea program hii kwa mikono miwili, na tunalenga kutekeleza kwa vitendo na lengo letu ni azma hiyo iweze kutimia.
Amesema Mkoa wa Dr es Salaam una fursa nyingi zikiwemo za kilimo cha mbogamboga, ufugaji wa kuku, Samaki ni kwenye mabwawa ya kuchimba.
“Kwa sasa mkoa huu unajipanga kuendelea kujenga masoko makubwa ya kisasa katika kila wilaya na kama mnavyojua kwamba soko la Kariakoo linajengwa la kisasa zaidi na lipo katika hatua za mwisho,” amesema RC Chalamila.
Ameongeza kwamba Rais Samia ana ndoto za kuwawezesha wanawake wa nchini kiuchumia kwa kutaka kuwaunganisha na biashara na fursa zitokanazo na miradi ya kimkakati unayoendelea hapa nchini.
Amesema Serikali ya Mkoa itaendelea kuwahamasisha wakinamama katika juhudi za kutaka wajihusishe na shughuli za ujasiriamali kwa kutumia fursa zilizopo za miundombinu ya reli, barabara na kiwanja cha ndege kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Beng`i Issa alisema baraza lake kupitia programa ya Imarisha Uchumi na Mama Samia imekuja kuwakwamua wanawake, vijana na makundi maalumu kufanya shughuli za kijasiriamali.
“Baraza la linatambua Mkoa wa Dar es Salaam mkoa unahitaji maeneo kwa ajili ya kusindika mazao yao, kuwa na masoko (super market) ili wateja waweze kwenda kununua bidhaa zilizotengenezwa hapa nchini,” amesema.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba