October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashekh Dodoma wakana kauli ya Sheikh Ponda

Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online,Dodoma

SHEIKH Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mustapha Rajab amesema kauli iliyotolewa na Sheikh Ponda Issa Ponda kuwa waumini wote wa dini ya kiislamu wamekubaliana kumchagua Tundu Lissu ni ya kwake binafsi na hakuna makubaliano katika uchaguzi Mkuu ujao.

Wiki iliyopita katika mkutano uliofanyika jijini Dodoma wa Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Sheikh Ponda alisema waislamu wote wamekubaliana kumchagua Lissu kuwa Rais katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa baada ya kumalizika kikao cha Baraza la Masheikhe wa Mkoa wa Dodoma,Sheikh Mustapha amesema kauli aliyoitoa Ponda sio ya waislamu wote, bali ni kauli yake yeye mwenyewe kwa maslahi yake binafsi.

Amesema hakuna mahali popote ambapo waislam wamekubaliana suala hilo na kama lingekuwepo, basi msemaji mkuu ambaye angepaswa kulitolea tamko ni Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuber na siyo vinginevyo.

Sheikh Mustapha amewataka masheikh na viongozi wote wa dini kwa ujumla kurejea makubaliano yao ya kuombea na kuwahimiza wananchi kuenzi amani na utulivu nchini hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu.

“Tunalaani vikali tamko lililotolewa na Sheikh Ponda ,maneno yake yapuuzwe maana msemaji mkuu wa waislam ni Sheikh Mkuu wa Tanzania.” amesisitiza

Ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha siku ya kupiga kura wanakwenda kupiga kura na kumchagua kiongozi wanayeona atawafaa katika kuwaletea maendeleo