Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeamua kutumia Ndege Mpya ya Kisasa ya Mizigo Boeing 767-300 inayomilikiwa na Kampuni ya Ndege ya Air Tanzania kusafirisha shehena ya chanjo zilizotoka India kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kupakia shehena hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mmoja kati ya wadau wa Usafirishaji Mizigo wa Anga Bw. John Lupembe amesema sababu ya kutumia ndege hiyo ni kutokana na ubora wa huduma unaotolewa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) pamoja na uwezo wa ndege hiyo kuweza kubeba bidhaa zenye mahitaji tofauti tofauti.
Lupembe ameongeza kuwa ndege hii imepunguza adha kubwa ya usafirishaji wa mizigo hapa nchini ikiwemo bidhaa za aina ya chanjo ambazo uhitaji kiwango maalumu cha joto ili kulinda ubora wake.
Kwa upande wa ATCL, Meneja Biashara Edward Nkwabi amesema wanauzoefu wa kutosha katika kusafirisha shehena za madawa na chanjo.
Ameeleza hapo awali, walikuwa wakitumia ndege yao ya masafa ya mbali ya abiria Boeing 787-8 Dreamliner kusafirisha mizigo ya aina hiyo.
Nkwabi amesema ATCL wataendelea kutoa Kipaumbele katika kuwezesha harakati za Mashirika ya Umoja wa Mataifa kama sehemu ya mchango ili kufanikisha huduma za ukozi duniani.
Meneja huyo amesema wasafirishaji wa mizigo hawana budi kutumia fursa hiyo iliyoletwa na Serikali katika kuhakikisha wafanyabiashara wa ndani ya nchi wanaendelea kunufaika.
“Nia ya ndege hii ilikuwa ni kuchochea bidhaa zetu za ndani kusafirishwa kwenda nje, hivyo tunahitaji ushirikiano wa Serikali kuhakikisha wanaongeza thamani ya bidhaa zao kwa kuwa zinaondokea hapa hapa,” amesema Nkwabi.
Amesema licha ya shirika hilo kuanza biashara ya usafirishaji na ushindani uliopo sokoni, bado ndege hiyo ya mizigo inatoa huduma kiasi cha kuendelea kuaminiwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo UNICEF.
Naye, Mbarouk Mbarouk, Rubani Mtanzania anayeongoza ndege hiyo, amesema leo wanakwenda Kinshasa na Tani 26 za mzigo pia watachukua mizigo mingine jijini Nairobi na kurudi Tanzania.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa