Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Butamo Ndalahwa na watumishi wa Halmashauri hiyo wameshiriki kufanya usafi katika kituo cha afya Mlandizi pamoja na kutoa misaada kwenye vituo vya kulelea watoto.
Shughuli hizo ambazo zimefanyika juzi mjini Mlandizi ni kati ya vitu vilivyofanywa na Halmashauri hiyo katika maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru anbayo kilele ni Desemba tisa.
Akizungumza baada ya kufanya usafi na kugawa misaada kwa wanawake wajawazito waliokuwa wanapata huduma katika Kituo cha Afya Mlandizi Ndalahwa alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan maboresho yanayoendelea kufanyika kwenye sekta ya afya.
Alisema uwepo wa dawa na watoa huduma kwenye kituo hicho imesaidia kwa kipindi cha mwaka mzima kutokuwa na taarifa za vifo kwa Mama na mtoto huku huduma nyingine zikiwa zimeboreka.
“Katika maadhimisho haya tuliamua kufika katika kituo hiki cha afya na kutenbelea vituo vinavyolea watoto wanaotoka kwenye mazingira hatarishi tuwasikilize vikwazo wanavyokumbana navyo Serikali ione namna ya kusaidia kuvitatua” alisema Mkurugenzi huyo.
Mganga mfawidhi kituo Cha afya Mlandizi Dk.Sebastian Misoji alimshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri kwa namna ya ufuatiliaji na kushiriki kutatua vikwazo jambo ambalo limesababisha kituo hicho kutoa huduma bora.
Akishukuru baada ya kupokea msaada Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto cha Upendo Erick Ouma alimshukuru Mkurugenzi kwa kukumbuka kituo hicho na kuwapatia msaada.
Ouma alisema kwasasa kituo hicho kina watoto 19 na wapo ambao wanasoma vyuo, sekondari na shule za msingi.
Vituo vilivyopatiwa misaada hiyo ni pamoja na Vijaliwa vingi, Upendo na Masjid Noor ambavyo vyote vipo mjini Mlandizi vikiwalea watoto wanaotoka katika mazingira hatarishi na yatima.
More Stories
Simbachawene:Waombaji wa ajira jiungeni na Mfumo wa Ajira Portal
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki