Na Elibariki Mafole, TimesMajira Online,Kagera
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Mashauri Ndaki ameumaliza mgogoro wa ardhi kati ya wananchi waliovamia kwenye vitalu katika Ranchi ya Kagoma na wawekezaji ambao wanamiliki vitalu hivyo.
Waziri Ndaki ameumaliza mgogoro huo baada ya kuwasikiliza wananchi na wawekezaji kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Rutoro wilayani Muleba Mkoa wa Kagera.
Akizungimzia kuhusu mgogoro huo, Waziri Ndaki amewaeleza wananchi kuwa maeneo hayo waliyoyavamia ni mali ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambayo tayari yalikuwa yameshakodishwa kwa wawekezaji wanaofanya shughuli za ufugaji hivyo walipaswa kuondolewa.
Lakini kutokana na busara za Rais Samia ameridhia eneo hilo lipimwe na wananchi wabakizwe kwenye vijiji vinne vilivyopo ambavyo ni Kijiji cha Rutoro, Byengeregere, Chobuheke na Mishambya vilivopo katika Kata ya Rutoro.
“Ninyi wananchi mnatakiwa kumshukuru sana Rais Samia kwa maamuzi yake ya kuwabakiza katika maeneo haya. Lakini niwasihi kuwa watulivu wakati wa zoezi la upimaji wa maeneo na kutoa ushirikiano kwa wataalam watakao kuja kutekeleza zoezi hilo,” alisema Waziri Ndaki.
Vilevile amewataka wananchi kutoendelea kuvamia maeneo mengine katika ranchi hiyo kwani wakifanya hivyo kwa sasa watachukuliwa hatua. Waziri Ndaki pia ametoa onyo kwa wananchi wenye tabia ya kuuza maeneo hayo wakati wao wenyewe hawajamilikishwa.
Pia kwa upande wa wawekezaji hao amewahakikishi kuwa zoezi hilo la upimaji wa maeneo halitaathiri shughuli zao za ufugaji kwa kuwa utawekwa utaratibu mzuri. Vilevile amewaeleza kuwa maamuzi hayo ya kupima maeneo na kuweka alama za mipaka yatasaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi na kufanya pande zote kuishi kwa amani.
Katika mkutano huo yametolewa malalamiko kuwa wafugaji wanalisha mifugo kwenye mashamba yao na kuwasababishia hasara. Kutokana na hilo Waziri Ndaki aliwaagiza wafugaji hao kuacha tabia hiyo kwani ni moja ya vitu vinavyosababisha tatizo la njaa kwa wananchi na kuleta migogoro baina ya pande zote mbili.
Vilevile wawekezaji wametakiwa kuhakikisha wanayatumia maeneo waliyopewa kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo. Aidha, uongozi wa wilaya ya Muleba umetakiwa kuweka utaratibu utakaotumika kuwaondoa wavamizi kwenye vitalu ambao wameingiza mifugo yao wakati hawajamilikishwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Muleba,Toba Nguvila amemuhakikishia Waziri kuwa maelekezo aliyoyatoa watakwenda kuyasimamia kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Kagera na uongozi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).
Kutokana na uamuzi uliochukuliwa wa kupima maeneo hayo kwenye ranchi ya Kagoma, wawekezaji na wananchi wote wameonesha mtazamo chanya kwani hata wao wenyewe hilo ndio wameliona ndio suluhisho.
More Stories
Mwalimu adaiwa kumfanyia ukatili mwanafunzi
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu