December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nchimbi ahitimisha ziara kwa kusikiliza kero za wananchi Arusha

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Arusha

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, amewaaga wananchi wa Arusha kwa kusikiliza kero na changamoto zao ikiwa pamoja na kero za wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyopo Mkoani Arusha kutopatiwa fedha za mikopo (Boom) kwa kipindi cha miezi sita.

Kero nyingine ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara, Mabalozi wa CCM kutolipwa posho na malalamiko ya uwepo wa migogoro ya ardhi baina ya wananchi.

Akizungumaza na wananchi wa Usariver Wilaya ya Arumeru, wakati akihitimisha ziara yake Mkoani Arusha na kuendelea na ziara yake Mkoani Kilimanjaro, Dkt. Nchimbi akijibu kero ya wanafunzi wa vyou Mkoani humo,amesema ndani ya mwezi huu kero hiyo itakuwa imetatuliwa na wanafunzi kupatiwa mikopo yao.

Amesema, anahitaji kupata muda wa kukuhakikishia kuhusu suala hilo kwani kuna wakati fedha zinakuwa zimeshatolewa lakini changamoto huwa kwenye mifumo ya kibenki.

“Nahitaji muda wa kujiridhisha kuhusu hii changamoto ya wanafunzi wa vyuo vya mkoani hapa, kwani kuna wakati fedha zinakuwa zimeshatolewa lakini shida inakuwa kwenye mifumo ya kibenki, lakini niwatoe shaka tatizo hilo litatatuliwa ndani ya mwezi huu kwani CCM haishindwi jambo”,amesema Nchimbi.

Akizungumzia changamoto zingine amewatoa hofu wananchi  kuwa zitatatuliwa huku akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuzitatua changamoto zingine.

Kwa upande wake, Katibu wa  (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amewataka wananchi kuendelea kuwa na Imani na chama na kudai kuwa chama cha CCM kipo kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020/2025.

“Niendelee kuwasisitizia wananchi wa Mkoa wa Arusha nyie ni wajanja na hampo tayari kuyumbishwa na wapotoshaji CCM ipo kwa ajili ya wananchi wote na itaendelea kutekeleza Ilani ya Chama kwa kuwaletea miradi ya maendeleo kila sehemu,”amesema Makalla.

Naye Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Hamid Abdalla, amesema ni vyema wananchi wakaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususani katika kumuombea pindi anapokuwa nje ya nchi kwa safari hizo zipo kwa ajili ya manufaa ya wananchi kwa ujumla.