Na Penina Malundo,Timesmajira
NCHI za Afrika zinaendelea kuwa na mabadiliko na maendeleo madhubuti kuanzia ngazi ya chini hadi juu kwa kujenga imara uwezo na sera nzuri zinazozingatia maslahi ya kitaifa.
Katika kujenga sera hizo viongozi wastaafu wa Afrika wamekuwa na dhamira ya kutumia teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kuleta mageuzi ya kina katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030 kwa nchi za Afrika.
Teknolojia za kidijitali na kukuza uvumbuzi kunaweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha utoaji wa huduma katika nchi za bara la Afrika.
Ni vema kukabiliana na changamoto mbalimbali lakini ni vema kukubali uvumbuzi kwa nchi za Afrika na kutengeneze njia ya kufikia Afrika endelevu na yenye mafanikio kupitia njia za Teknolojia za kidijitali.
Yoweri Museveni Rais wa Uganda, akizungumza katika Kongamano la 8 la Uongozi wa Afrika (ALF), lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi ambalo lilijadili hali ya sasa ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) katika nchi za Afrika huku likibaini changamoto kuu na vikwazo vinavyozuia maendeleo.

Museveni anasema nchi za Afrika zinapaswa kuendelea kuleta mabadiliko yatakayoanzia ngazi ya chini kujenga uimara wa uwezo na sera nzuri zinazozingatia maslahi ya kitaifa.
Anasema kupitia SDGs ni muhimu viongozi kuhakikisha wanapambana kuondoa vikwazo vya kimkakati vinavyozuia mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika bara la Afrika.
“Ni muhimu viongozi kutumia fursa ya kongamano hili na kuweka mazingira mapya yatakayowezesha ‘Afrika Kwanza’ katika juhudi za kutimiza Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs),” anasema Rais Museveni
Kwa upande wa nchi yake, anasema uchumi wao umejengwa katika hatua tano tangu walipoanza kuendesha serikali, moja ni namna ya kurejesha kidogo, kupanua uchumi wa zamani wa kikoloni, kubadilisha uchumi, kuongeza thamani kwenye uchumi na kuelekea kwenye uchumi wa maarifa.
Naye Mratibu Msaidizi wa ALF na Waziri Mkuu wa Zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Hailemariam Desalegn anasema kuwa Afrika inakabiliwa na fursa lakini pia changamoto katika kufikia malengo ya SGDs, kama vile uhaba mkubwa wa ufadhili na hivyo rasilimali kubwa zinahitajika kuziba pengo hilo.
Anasema njia mbadala za kufadhili SDGs lakini wakati huo huo anatoa wito wa kuimarishwa kwa utawala na taasisi, uwazi, utawala wa sheria, kupambana na rushwa na kuzuia mianya haramu ya fedha.
“Hili, linapaswa kwenda sambamba na nguvu kazi imara, uhakika endelevu wa chakula, nishati ya uhakika na kuimarisha ushirikiano katika biashara na uchumi mpana katika bara lote kwa kukubali kupunguziwa kwa uhuru wa nchi binafsi na kukumbatia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA),” anasema na kuongeza
“Kama inakuwa vigumu kufanya biashara na uchumi ulioimarika zaidi wa magharibi, ni vyema kuimarisha biashara za ndani, kutumia teknolojia na uvumbuzi, kuhamasisha rasilimali na kupunguza misaada ya kigeni na Misaada Rasmi ya Maendeleo (ODA).” anasema

Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika, Antonio Pedro anasema katika utekelezaji wa SDGs, ni muhimu kuelewa kuwa ukosefu wa ajira si suala la kiuchumi tu bali pia ni tishio kwa amani na jaribio kwa mfumo wao wa kiuchumi, akiongeza kuwa sekta binafsi haipaswi kuwekeza tu kwa faida bali pia kwa lengo.
Anasema kuwa bara la Afrika linahitaji mfumo mpya wa SDGs,katika kuondoa vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru kuna uwezo wa kuongeza biashara ya ndani ya Afrika kwa asilimia 45 katika muongo ujao na kwamba wakati uchumi wa kimataifa wa Akili Mnembe unatarajiwa kufikia dola trilioni 1.8 ifikapo mwaka 2030, huku Afrika ikiwa bado na asilimia moja tu ya hiyo.
Mratibu Mkuu wa FAO kwa Afrika Mashariki, Mafa Chipeta, anasisitiza mbinu ambayo ni chaguo bora zaidi na iliyolenga upya katika utekelezaji, akibainisha kuwa ikiwa bara litachukua SDGs zote kwa mara moja, linaweza kujiminya sana.
Msingi wa hoja yake ulihusishwa na ukweli kwamba bara la Afrika lina asilimia 17 hadi 18 ya idadi ya watu duniani lakini likiwa na asilimia 2 tu ya Pato la Taifa la Dunia na biashara, likiwa na alama ya asilimia 3 kwa viashiria vingi vya kiuchumi na likiwa na chini ya asilimia 0.5 tu kwa teknolojia mpya muhimu.

Anaonya zaidi kuwa wizara za biashara za Afrika zina utamaduni wa kupuuza biashara kubwa ya ndani kuliko biashara ya nje ambayo inawaacha wafanyabiashara wanyonyaji kuwaibia wakulima wadogo na inaendelea kutoa ruzuku kubwa kwa uchumi wa dunia kwa kuuza malighafi, ambayo haijasindikwa na yenye thamani ndogo kwa bei rahisi na kuja kununua tena bidhaa kwa bei za juu.
Anasema kuwa bara linahitaji kupunguza utegemezi kutoka wafadhili kwa kutenga fedha zake ili wafadhili wasiwe mbadala wa nafasi ya dhamira ya ndani.
Naye Rais wa Zamani wa Jamhuri ya Tunisia Dkt. Mohamed Moncef Marzouki anatoa wito kwa Afrika kujitegemea kupitia biashara ya ndaniya wao kwa wao, ambazo zinapaswa kutanguliwa kwa kuwa na serikali za kidemokrasia, huru na zisizojihusisha na rushwa.
Makamu wa Rais wa Zamani wa Uganda, Gilbert Bukenya, anasema Afrika inapaswa kuwa na uongozi bunifu ambao utawakwepa wale wanaotaka kuiendesha kwa maslahi ya nje na badala yake kuendesha ajenda yake yenyewe ya mabadiliko.
Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje, Sam Kutesa, anasema SDGs zilikuwa matarajio sahihi na kwamba kilichohitajika kwa bara hili ni kubuni hatua mpya za kufadhili utekelezaji wake, kama vile kutumia rasilimali asili za ndani na ufadhili kutoka sekta binafsi.
More Stories
Umuhimu wa kujadili mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya watoto
Mo Dewji na Urithi anaoujenga ,unavyoenda mbali zaidi ya mafanikio binafsi
Tanzania yaadhimisha siku ya hali ya hewa,kwa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma zake.