November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nchi za Afrika Mashariki kunufaika na vifaa vya kisasa CBE

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kisasa kwenye idara yake ya vipimo na viwango hususan kwenye upimaji wa mafuta ya vyombo vya moto.

Hayo yamesemwa jana chuon hapo na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Tandi Lwoga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maboresho yanayofanywa na chuo hicho.

Amesema katika siku za hivi karibuni, CBE imekuwa kwenye safari ya maboresho makubwa ya maabara zake, ikichochewa na dhamira yake ya kutoa elimu bora zaidi kivitendo kwa wanafunzi wa chuo hicho.

“Nafurahi kushiriki nanyinyi habari za uwekezaji mkubwa ambao bila shaka utaboresha utoaji wetu wa elimu katika fani hii ya vipimo na viwango hasa katika eneo la upimaji wa mafuta ya vyombo vya moto (Dizeli, petroli, mafuta ya ndege), pamoja na Mafuta ya taa kwa kampasi zetu za Dar es Salaam na Dodoma,” amesema.

Aidha, Profesa Lwoga amesema mnyororo mzima wa uuzaji wa mafuta una jukumu muhimu katika uchumi wa nchi na ni uwanja unaoendelea kubadilika mara kwa mara.

“Ni muhimu kwamba wanafunzi wetu wa viwango na vipimo wapokee mafunzo ya kisasa na ya kina ili kufaulu katika sekta hii kwa kuzingatia lengo hili, chuo kimefanya uwekezaji mkubwa katika vifaa vipya vya kozi zetu za pampu ya mafuta,” amesema.

Profesa Lwoga alisema vifaa hivyo vinajumuisha mfumo mzima wa pampu za mafuta, utakaoundwa kwa mfano wa kituo cha mafuta kwa kuweka matenki ya ardhini ya kuhifadhia mafuta.

Amesema pia wataweka pampu za mafuta zenye mikono minne, mfumo wa kupima ujazo moja kwa moja na vifaa vya uhakiki wa upimaji wa ujazo katika vituo vya mafuta.

Akizungumzia umuhimu wa mfumo huo katika jamii, Profesa Lwoga amesema maabara hizo zitatumika kama maeneo ya kujifunza ambapo wanafunzi wa CBE wanaweza kupata uzoefu wa vitendo na kukuza ujuzi muhimu unaohitajika katika tasnia.

Amesema maabara hizo zitatoa fursa kwa wanafunzi wa kozi fupifupi mfano wauzaji wa mafuta na mafundi pampu kupata eneo sahihi la kujifunzia kivitendo.

Amesema maabara hizo zitasaidia kukuza utaalam vipimo nchini na nchi za ukanda wa Afrika mashariki na kati na hivyo kuendelea kuchagiza ubora katika mnyororo/ufuatiliaji wa vipimo ili kuhakikisha mlaji anapata anachostahili.

“Lakini na muuzaji anapata anachostahili kama wenzetu TBS wanavyosimamia viwango hivyo na Wakala wa vipimo wanavyosimamia utekelezaji wa sheria ya vipimo,” amesema.

Amesema maabara hizo zitasaidia kullisha soko la ajira (viwanda vya uzalishaji na uchakataji) zao lililo bora zaidi katika tasni ya viwango na vipimo na kusaidia kutoa ushauri wa kitaalam kivitendo unaoendana na mahitaji ya soko katika mnyororo ya upimaji na uuzaji wa mafuta.

Profesa Lwoga amesema zitasaidia pia kutoa mafunzo mtambuka ya kitaalam na kivitendo kwa jamii katika mashaka yao juu ya uuzwaji wa mafuta

“Tunatarajia kupokea vifaa vingine vitakavyojumuisha upimaji wa mita za maji na matenki ya mafuta. Hivyo Ninawahimiza wanafunzi wote kutumia vyema rasilimali hizi, kujitahidi kupata matokeo bora, na kutekeleza ndoto zao katika uwanja wa teknolojia ya vipimo inayokua kwa kasi sana hivi sasa.