January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nchi haitapata changamoto ya kukosekana kwa chakula – Bashe

Na David John TimesMajiraonline

NAIBU waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kuwa nchi haitapata changamoto ya kukosekana kwa chakula licha ya kukosekana kwa mvua na kuwepo Kwa ukame ambao utapunguza uzalishaji.

Bashe ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na chombo kimoja cha Habari nchini kwa njia ya simu ambapo amebainisha wazi kuwa wizara kupitia taasisi zake imechukua hatua stahiki kuhakikisha wanakabiliana na changamoto ya chakula.

Naibu waziri huyo amelazimika kufafanua hayo baada ya hivi karibuni kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakulima wakidai kuwa kutokana na hali ya ukame na ukosefu wa mvua unaweza kuathiri uzalishaji.

Kutokana na hali hiyo ya ukame pamoja na kuathiri sekta ya kilimo katika baadhi ya maeneo, pia imesababisha kuwepo kwa uhaba wa maji hali ambayo inaleta athari kwa Jamii hususani mkoani Dar es salaam.

“ Sisi kama Serikali na wizara tunajiamini kwamba nchi yetu haitapata tatizo la chakula,licha yakwamba ni kweli mvua zimepungua, kuna maeneo ambayo yatapata chini ya wastani, mengine yatapata wastani, “amesema

Nakuongeza kuwa “tunaweza tusipate uzalishaji kama tuliopata mwaka huu, lakini hatuwezi kuwa na njaa kama nchi, kwa sababu tunaamini tutapata chakula kitakachotutosheleza kama nchi,” amesisitiza

Bashe alifafanua kuwa kuna kanda zingine hazitapata mvua za kutosha ila zipo ambazo zitapata mvua na kuwezesha kuzalisha mazao mengi.

Amesema Serikali kupitia wizara ya kilimo imeelekeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) wamenunua chakula cha kutosha hivyo hofu ya kupata njaa haitakuwepo.

Bashe amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetoa shilingi bilioni 117 ambazo zina uwezo wa kununua zaidi ya tani laki mbili.

“Serikali imetoa shilingi bilioni 50 kwa NFRA na CPB na wanaendelea kununua chakula, hivyo niwahakikishie Watanzania kuwa hakutakuwa na uhaba wa chakula,” amesema.

Amesema hifadhi zilizopo zinaweza kuhifadhi tani 500,000 ambapo kwa sasa zaidi ya tani 300,000 zipo katika hifadhi zilizopo.

Amemaliza kwa kuwataka wakulima ambao maeneo yao mvua zinanyesha kuendelea na kilimo ili kuweza kusaidia nchi kuzalisha chakula kingi kwa matumizi ya majumbani na biashara.