November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NBC kuimarisha ushirikiano na wateja Dodoma

Mkurugenzi wa wateja wakubwa wa NBC, Bw. James Meitaron (pichani) akizungumza na wageni waalikwa wakiwemo wateja wa benki hiyo na wadau wengine wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo ikilenga kuboresha mahusiano na wateja sambamba na kutambulisha huduma mpya za benki hiyo ikiwemo huduma ya NBC Connect mahususi kwa taasisi na mashirika mbalimbali. Kupitia hafla hiyo benki hiyo iliweza pia kupokea mrejesho kutoka kwa wateja na wadau hao kuhusu huduma zake mbalimbali.

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Benki ya Taifa ya Biashara kupitia timu ya kitengo cha Biashara na Uwekezaji (CIB), imefanya Ziara ya kukuza ushirikiano pamoja na ubunifu kwa wateja katika tasnia ya Benki Mkoani Dodoma.

Aidha, katika ziara hii Timu ya NBC ilipata nafasi ya kumsalimu Mhasibu Mkuu wa Serikali Ndg.Leonard Mkude katika Ofisi za Wizara ya Fedha Dodoma pamoja Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA Mhandisi Victor Seff katika Ofisi za TARURA zilizoko Mtumba Dodoma

Ushirikiano baina ya taasisi za kifedha na wateja ni muhimu kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya mazingira ya ubunifu na maendeleo ya kiteknolojia. Hivyo benki ya NBC imefanya ziara hii kama sehemu ya kuwasikiliza wateja na kuboresha huduma ili kukidhi mahitaji yao.

Akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni, iliyoandaliwa na NBC katika viwanja vya Collina Hoteli ambayo ilihudhuriwa na baadhi ya wateja. Mkurugenzi Mtendaji wa kitengo cha biashara na uwekezaji NBC, James Meitaron, Amesema “Tunaamini kuwa ufunguo wa kuwa mtoa huduma wa kipekee ni kuelewa mahitaji na matakwa ya wateja wetu. Hivyo kupitia ziara hizi tunapata mapendekezo na ushauri wenye suluhu zenye ubunifu wa kuboresha uzoefu wa kibenki kwa ujumla”

Wateja waliohudhuria hafla hii, wameonyesha kufurahishwa na mkakati huu wa NBC connect wenye lengo la kugusa biashara zao. Ambapo wamepata fursa ya kueleza changamoto zinazowakumba na kutoa ushauri ambao utarahisisha zaidi shughuli na huduma za kifedha mkoani humo.

Benki ya taifa ya biashara NBC wameahidi kuendelea kujali na kusikiliza matakwa ya wateja wao ambapo hivi karibuni wanatarajia kuendeleza ziara hiyo katika mkoa wa kanda ya ziwa ambao ni Mwanza pamoja na mkoa uliopo kanda ya kaskazini Arusha.