Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka Wakandarasi wote watakaohusika na ujenzi wa mkongo wa Taifa kuhakikisha wanafanya kazi hiyo kwa ubora na umakini mkubwa na kuzingatia viwango vya ubora.
Nakusema yeyote atakayebainika kufanya vibaya atakuwa amejifungia kufanya kazi na Wizara na serikali nzima.
Waziri Nape amesema hayo jijini hapa leo katika hafla ya kuzungumza na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa kilomita 4,442 za mkongo huo wa taifa,ambapo amesema kwasasa serikali ipo kwenye mchakato wa kuhamishia shughuli zote za mkongo huo kwenye Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL).
“Kama kuna kazi za kucheza nazo basi ni za Wizara nyingine, lakini sio Wizara ya habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa sababu itawafanya kukosa kazi za wizara hiyo na Serikali nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
“Inabidi maneno mengine magumu tuyaseme na kwenye hili itabidi niwe mkali kidogo…Kazi hii tunayoikamilisha Desemba 2022 itatuambia nani twende naye ili tusipasuane vichwa mbele ya safari,
“Mimi siamini katika kumpiga mtu buti kabla ya kumwambia, mwambie kwanza, sasa imebidi niyaseme haya vizuri tumeweka fedha ya umma kwenye hii miradi lazima ifanyike kwa ubora na kwa wakati, kazi hii ya mbele ni kubwa zaidi na fursa zipo ila zitapimwa kwa kazi uliyopewa nyuma…Niwahakikishie mkifanya kazi vizuri mtafurahia kufanya kazi na sisi lakini mkifanya vibaya mtajutia kufanya kazi na sisi,”amesema Waziri Nape.
Pamoja na hayo Waziri huyo amesema kwa Mwaka 2022/23 serikali inatarajia kujenga zaidi ya kilomita 1600 na vituo vipya 15 na lengo ni kufika Wilaya 81 na urefu wa kilomita 14,361 sawa na asilimia 95 ya lengo kubwa la kufikia kilomita 15,000 ifikapo Mwaka 2025.
“Kuna umuhimu kwa takwimu hizi kuwepo na ushirikiano wa sekta binafsi na serikali pekee haiwezi kumaliza, nitoe wito serikali ya awamu ya sita inaamini kwenye ushirikiano wa serikali na sekta binafsi katika kuendesha shughuli zake, yawezekana mmekutana na mawimbi mbalimbali niwahakikishie yametulia tupo tayari kushirikiana na mfanye kazi sawa sawa kwa kuwa mna mchango mkubwa kwenye maendeleo,”amesema.
Amesema tangu kuanza kujengwa kwa Mkongo huo mwaka 2009, ujenzi wake umefikia kilomita 8,319 na zaidi ya Sh.Bilioni 670 zimetumika na una vituo kwenye mikoa 25 Tanzania bara na Wilaya 43 kati ya 139 sawa na asilimia 30.9 zimefikiwa na kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
“Mwaka 2021/22 zilitengwa Sh.Bilioni 170 kwa ajili ya kujenga kilomita 4,442 na kuongeza uwezo kutoka 200G kwenda 800G, jumla ya mikataba 22 ilisainiwa na ilihusisha kampuni nane, takwimu zinaonesha kati ya kampuni hizo sita ni za watanzania kazi hii inapaswa kuisha Desemba 2022, ikikamilika yote tutakuwa tumefikia kilomita 12, 761 kati ya 15,000 za lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025,”amesema.
Waziri Nape ameongeza kuwa mkongo ni muhimu katika kujenga uchumi wa kidigitali na kwamba serikali imeahidi itapitia baadhi ya sheria, sera na kanuni ili kujenga uchumi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo,Mlembwa Mnako amesema kuwa mkongo huo umesaidia kupunguza gharama za kusafirisha mawasiliano kwa njia ndefu ambapo awali walikuwa wakitumia satelaiti.
“Mwaka 2005 serikali ilifanya uamuzi thabiti kwamba tuwe na mradi wa mkongo wa taifa na kati ya mwaka 2005 na 2007, ilifanyika tathmini ya mkongo uweje na kutafuta gharama za awali za kutekeleza mradi huu, na mwaka 2008 ambapo serikali ilipata fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa benki ya Exim China,”amesema.
Pia ameeleza kuwa Mwaka 2009 mradi huo ulipoanza kutekelezwa zilijengwa kilomita 4,330 na ilifungwa mitambo yenye uwezo wa 10G na baada ya kipindi hicho serikali ilitafuta fedha za kujengwa kilomita zingine 3,630 na hivyo kuwa na kilomita zaidi ya 7,000 zilizojengwa.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais