December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nancy Foundation Tanzania yawakumbuka watoto wa mitaani Shinyanga

 

Na Suleiman Abeid,Timesmajiraonline,Shinyanga

WITO umetolewa kwa wazazi na walezi wa watoto katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto wao kwa kuwalea katika maadili mema na wahakikishe wakati wote wanawalinda ili wasitendewe vitendo vya ukatili.

Wito huo umetolewa na wadau wa kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wakati wa hafla fupi ya kukabidhi misaada ya sare za shule na madaftari kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao umetolewa na Taasisi ya Nancy Foundation Tanzania yenye makazi yake Manispaa ya Shinyanga.

Katika hotuba yake kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Wingilwa Kitila ambaye pia ni Ofisa elimu Taaluma katika Manispaa hiyo, amesema vitendo vya ukatili dhidi ya watoto bado ni tatizo katika maeneo mengi ya Mji wa Shinyanga.

Kitila amesema hivi karibuni kumeripotiwa tukio la mtoto mmoja kutendewa ukatili na mtu wa karibu ndani ya familia yao ambaye ni mjomba wake hali inayoonesha bado juhudi zinahitajika zaidi katika kuielimisha jamii ili iweze kuacha kuwafanyia ukatili watoto wadogo vinavyowaathiri wengi wao na kuwaharibia ndoto zao za maisha.

Amesema hivi sasa kuna kuna kundi kubwa la watoto wanaoishi mitaani wakizurura ovyo na kuokotaokota vyuma chakavu kwa lengo la kuuza ili wajipatie fedha za kujikimu kimaisha na mara nyingi huko mitaani na maeneo wanayolala hujikuta wakitendewa vitendo vya ukatili na watu wakubwa.

“Wiki iliyopita nilikuwa na kesi ya mtoto aliyetendewa vitu vya ajabu na mjomba wake, ambavyo vinasikitisha, mama anahangaika kutafuta ili alete kwa ajili ya mtoto apate lakini akamwacha mtoto na mjomba wake na mjomba naye akaendelea kumfanyia mambo mengine, ninaomba sisi jamii tubadilike, tuwasaidie watoto hawa hasa wanaoishi mitaani,”

“Naamini miongoni mwa watoto hawa kuna Rais, waziri mkuu, wakuu wa mikoa na wilaya, madaktari na viongozi wengine mbalimbali watakaokuja kuongoza nchi yetu hii, sasa tuwasaidie kimavazi, kiroho na hata kwa chakula, ili ndoto zao zitimie ni juu yetu jamii tuwalee, kwa mitaani ukweli haiwezekani,” ameeleza Kitila.

Kwa upande wake Ofisaustawi wa Jamii katika Manispaa ya Shinyanga, Lemiflora Nyalaja amesema hali ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika manispaa yake bado ni kubwa na hivyo jamii inapaswa kusimama kidete kupiga vita vitendo hivyo.

Nyalaja ameipongeza Taasisi ya Nancy Foundation Tanzania kwa juhudi inazozionesha katika kuwakusanya watoto wanaoishi mitaani na kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo kuwarejesha katika familia zao na wengine kuwaunganisha na Kanisa la Hosana la mjini Shinyanga ambako wanapatiwa elimu ya kiroho.

“Kwa ushirikiano na Taasisi hii ya Nancy Foundation ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tumefanikiwa huko kuwapata watoto wapatao thelathini wakiwa katika makundi mawili waliokuwa wakiishi mitaani ambapo kundi la kwanza ni la watoto wanaouzurura tu mitaani lakini wana wazazi wao,”

“Kwa hawa wenye wazazi tumebaini wana uwezo wa kuwatunza lakini sababu ya maisha duni ndani ya familia wakaamua kuwaacha wazurure ovyo mitaani, tumewasiliana nao kuona jinsi gani watawalea watoto wao, pia kuna watoto sita ambao tumekosa wazazi ama walezi wao hivyo hawa wamepelekwa Kahama kwenye makazi ya watoto,” ameeleza Nyalaja.

Hata hivyo Nyalaja amesema hali ya ukatili dhidi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika Manispaa ya Shinyanga ni kubwa kutokana na kufanyiwa ukatili wa hali ya juu na kwa sababu ni watoto wanakosa sehemu ya kusemea kwa vile hata wazazi wao hawapo pamoja nao.

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Nancy Foundation Tanzania, Ezra Manjerenga amesema moja ya malengo ya Taasisi yake ni kuwakusanya watoto wanaoishi mitaani na kujaribu kuwakutanisha na familia zao ili waweze kuishi nao na kuwasimamia katika suala zima la wao kupata elimu.

Manjerenga amesema mbali ya kuwakusanya na kuwatambua watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu lakini pia Taasisi yake imekuwa ikiwapatia misaada mbalimbali ikiwemo mavazi, vifaa vya shule sambamba na kuwarejesha shule kwa wale ambao wamekuwa ni watoro wa rejareja.

“Katika vikao ambavyo tumekuwa tukivifanya na watoto hawa kwa kushirikiana na Ofisaustawi wa jamii tulibaini mambo mengi, baadhi yao walikuwa wameanza kufanyiana vitendo vya ulawiti, wengine wanalala kwenye mapagare, wao kwa wao hawaheshimiani, watoto hawa wanahitaji kutusamehe sisi wazazi,”

“Maana tumewaacha na kuwaona kuwa hawafai, lakini baada ya kuwaunganisha na kanisa hili la Hosana, wengi wao wamebadilika na kuonesha upendo miongoni mwao na hata kukirimiwa na kukumbatiwa na jamii jambo ambalo huko nyuma lilikuwa ni muhali kwao kulipata, tunaamini sasa watabadilika na kuwa watoto wema,” ameeleza Manjerenga.

Manjerenga ameendelea kufafanua kuwa kwa wale ambao tayari wamewabaini na kuwarejesha katika familia zao kwa sasa wanawapatia mahitaji muhimu ikiwemo kuwalipia fedha ya chakula na ya masomo ya ziada ili kubana muda wa wao kuzurura mitaani na pia pindi wanapokuwa hawako shuleni wanahudhuria masomo ya dini kanisani. Katika hafla hiyo Taasisi ya Nancy Foundation Tanzania imekabidhi msaada wa sare za shule, madaftari na mikoba ya kuhifadhia madaftari kwa watoto wapatao 30 ambao kwa sasa wanasimamiwa kwa ukaribu na Taasisi hiyo baada ya kuondolewa mitaani na kuunganishwa na familia za