November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri Masanja asisitiza ushirikiano katika utunzaji wa maliasili Afrika Mashariki

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kuimarisha juhudi za pamoja za kutunza maliasili zinazochangia katika maendeleo ya nchi hizo.

Ameyasema hayo leo Mei 20,2022 jijini Arusha katika Mkutano wa Nane wa Baraza la Sekta ya Mazingira na Maliasili .

“Afrika Mashariki ina utajiri wa maliasili ikiwemo misitu na wanyamapori ambao wanachangia katika maendeleo ya nchi za ukanda huo hivyo, usimamizi endelevu wa mazingira na maliasili ni muhimu ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kunufaika” Mhe. Masanja amesisitiza.

Ameongeza kuwa Sekta ya Utalii, upatikanaji wa maji na usalama wa chakula pia ni mambo ya muhimu ya kuyajadili katika mkutano huo ili kuangalia namna ya kunufaika kwa pamoja.

Mhe. Masanja amesema mkutano huo ni fursa ya pekee ya kujadili mikakati ya pamoja ya kuhakikisha kuna usimamizi mzuri wa mazingira na maliasili katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, amesema kuwa mkutano huo utajadili mikakati ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi zinazoathiri maendeleo ya kiuchumi ya kijamii akitolea mfano wa ukame.

Mkutano huo uliotanguliw na kikao cha Makatibu Wakuu wa Jumuiya hiyo, umehudhuriwa na baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda pamoja na nchi wanachama zilizoshiriki mkutano huo kwa njia ya mtandao ambazo ni Rwanda, Burundi na Sudan ya Kusini..