📌 Asisitiza utunzaji wa miundombinu ya umeme
📌 Kijiji cha Sunga wilayani Ushetu kupata umeme ndani ya siku Tisa
Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Judith Kapinga ameuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuongeza kasi ya kuwaunganishia umeme wananchi katika vijiji ambavyo tayari vimefikiwa na miradi ya usambazaji umeme ili kuleta tija.
Kapinga ameyasema hayo tarehe 1 Julai, 2024 wakati alipokagua miradi ya umeme katika Vijiji Vya Nimbo, Sunga na Nyawishi vilivyopo Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga.
“Haipendezi kuona mradi umefika katika kijiji na umekamilika lakini unakuta kaya tano au kumi zimeunganishwa, hii hailingani na nguvu iliyotumika kuufikisha mradi katika Kijiji, hivyo angalieni upya namna bora ya kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hii.” Amesisitiza Kapinga
Aidha, amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga Kuhakikisha wanaunganisha umeme kwenye taasisi ikiwemo Hospitali, Shule na miradi ya maji ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora za kijamii.
Pia, Mhe. Kapinga amewahakikishia wananchi wa kijiji cha Sunga kuwa watapata umeme ndani ya siku Tisa kuanzia sasa.
“ Wananchi wa Kijiji cha Sunga ifikapo tarehe 10 mwezi Huu mtakuwa mmepata umeme kwa sababu Mkandarasi ameshalipwa kila kitu na niahidi kuwa tutafikisha umeme kila sehemu ndani ya nchi kuanzia wilayani hadi vitongojini kwa sababu Rais Dkt. Samia ana nia ya dhati kuwapa huduma ya nishati watanzania wote.” Amesema Kapinga
Vilevile Kapinga ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanailinda miundombinu ya umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
” Nawaomba tutunze miundombinu hii ya umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu pamoja kutuletea tija katika shughuli zetu za maendeleo.” Amesema Kapinga
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro ameshukuru kwa kazi ya usambazaji umeme katika maeneo mbalinbali nchini na kumpongeza Mbunge wa Jimbo la ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani kwa kuwajali Wananchi kwa kuhakikisha anawapatia Maendeleo kwa Wakati.
More Stories
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao