November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri ‘amtumbua’ Meneja Mamlaka ya Maji Vwawa

Na Esther Macha,TimesMajira online,Songwe

NAIBU waziri wa Maji,Mhandisi Maryprsica Mahundi (Mb)ametengua nafasi ya Meneja wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Vwawa na Mlowo,Akiba Kibona kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake sambasamba na kutoa maji kwa mgao bila sababu za msingi .

Mkurugenzi wa maji na usafi wa mazingira Jijini mbeya Mhandisi ,Ndele Mengo akitoa maelezo namna wanavyochanganya dawa kwenye maji kwa Naibu waziri wa maji Mhandisi Maryprisca Mahundi

Mhandisi Mahundi amechukua uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg.Jen Nicodemus Mongella pamoja na kutembelea chanzo cha maji cha Mwantengu na kujionea chanzo cha maji kikisambaza maji kwa saa kumi na tano tu.

Naibu Waziri wa maji ametembelea Mkoa wa Songwe kuona miradi mbalimbali ya maji pamoja na kuzindua mradi wa maji wa Chapwa Mpemba Katete uliopo Wilayani Momba.

Hii pia Naibu waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akitembelea vyanzo vya maji Mkoani Songwe

Mhandisi Mahundi amesema kuwa Vwawa na mlowo kuna tatizo kubwa sana ambalo linatikisa na unafuu umekuja baada ya wakala wa usambazaji wa maji Vijijini (RUWASA).

“Mheshimiwa Rais John Magufuli ameleta pampu ya sh.mil.100 ili kuongeza ufanisi lakini bado mambo yaendelee kuwa magumu kwa wananchi kupata maji.

“Ndio maana unalaumiwa kutokana na maji kupotea na kushindwa kupata mapato kwa kufunga bila ya sababu ya msingi huu sio ubunifiu mzuri na kuonekana hautoshi kwenye nafasi hii,ndio maana imeonekana kubadilishwa mtu mwingine ili kuongeza ufanisi wa kazi ,nimejitahidi sana kukusikiliza kwenye vitendo upo vizuri shida ipo kwenye utekelezaji “amesema Mhandisi Mahundi.

Aidha Mhandisi Mahundi amesema kwa sababu meneja huyo amefeli katika nafasi yake licha ya rais kuleta fedha sh.mil.100 bado ameshindwa kufanya kazi ya kuhudumia jamii .

Hata hivyo alimwagiza Mkurugenzi wa Wakala wa Maji Vijijini Mkoa wa Songwe,Mhandisi Charles Pambe kuhakikisha kuwa changamoto ya maji katika Mji wa Mlowo na Vwawa kumaliza mgawo wa maji na yawepo masaa 24 na sio masaa 15 na kutotaka kusikia tena kero ya maji maeneo hayo.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya maji Vwawa na Mlowo ,Akiba Kibona amesema kuwa wanafanya juhudi kubwa kuhakikisha wanahudumia wananchi wote na kutekeleza maagizo ya waziri .

“Ni kweli kiutendaji naonekana sifanikishi lakini changamoto ninazosema ni za ndani Mh. Waziri lakini tunafanya juhudi kuwahudumia wananchi wetu kwa kiwango kinachotakiwa shida ninayoona ni tafsiri ya mazingira yetu kidogo inaweza kuwa tatizo upande wa kifedha,”amesema Mhandisi Kibona.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi,John Palingo amesema kuwa miaka ya nyuma miradi mingi ya maji ilikuwa shamba la bibi lakini kwa ujio wa RUWASA miradi mingi inatekelezwa na imekuwa na tija kwa wanachi na maji yanapatikana na imekuwa ikitekelezwa kwa fedha ndogo ukilinganisha na huko nyuma,wakala wa maji pia wamekuwa na ubunifu mkubwa wa kubaini vyanzo kwani huko nyuma ilikuwa inaonekana kama vyanzo hamna.