November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri aiagiza Serikali Zanzibar

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

NAIBU Waziri Wizara Maji, Nishati na Madini (WMNM) Zanzibar Shabaani Ali Othman ameagiza uongozi wa wizara hiyo kufikisha huduma ya maji safi na salama haraka katika Shehia ya Kizimbani Jimbo la Bububu, Wilaya Maghari ‘B’ ili kuwaondolea tatizo liliyopo.

Akizungumza na wakaazi wa eneo hilo, alisema haiwezekani wananchi wakose maji kwa muda wa miezi minne hivyo aliitaka Uongozi wa Wizara yake kuhakikisha wakaazi wa shehia hiyo wanafungiwa mashine ya kusukumia maji katika kisima cha rasilihema ili wapate huduma hiyo.

Alisema ikiwa changamoto kubwa ya maji katika eneo hilo inatokana na mashine ya kusukumia maji kuungua hivyo Wizara yake inajukumu la kufunga mashine nyengine ili  wananchi wapate huduma hiyo.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia wizara hiyo inatekeleza miradi mikubwa ya maji ili kuowandolea wananchi tatizo la maji safi na salama  ikiwa ni ahadi ya Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi   hivyo  sio muda mrefu miradi hiyo itakamilika.

 “Haiwezikani miundombinu ya maji ipite eneo hili wananchi wa Kizimbani wasipate maji, nimekuja na Katibu Mkuu na watendaji wa ZAWA ili wasikie malalamiko yenu na kuyafanyia kazi, hivyo mashine za maji zikifika tu Katibu Mkuu nakuagiza kisima cha rasilihema kifungwe mashine ya maji.” Alisema Othman.

Aidha alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) inajukumu la kurudisha miundombinu ya maji kwa wananchi ambayo imekatwa wakati wa ulazaji wa mabomba ya maji ikiwa ni utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji Zanzibar.

Pia Naibu waziri huyo aliwataka wakaazi wa eneo hilo kutunza miundombini ya maji ambayo imepita katika eneo hilo kwasababu miradi ya maji itakapo kamilika mwezi wa Disemba Mwaka huu, kusiwe na changamoto ya ukosefu wa miundombinu ya maji hali ambayo itapelekea usumbufu katika kukamilika kwa miradi hiyo.

Naye katibu Mkuu wa Wizara hiyo Joseph Kilangi alisema wizara yake inategemea kupokea mashine za kusukumia maji mwishoni  mwa mwezi wa Disemba, 2022.

Hivyo aliwahakikishia wakaazi  wa eneo hilo  watafungiwa mashine katika kisima chao hicho ili wapate huduma hiyo.

Alifahamisha  kwamba  mashine huwa zinafungwa kwa mujibu wa kisima, lakini atahakikisha wakaazi Shehia hiyo wanapata maji kwani wizara yake imejenga matangi  15 ambayo yatasaidia kuondoa tatizo la maji katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar ikiwemo jimbo la Bububu.

Hatua hiyo inatokana na malalamiko ya waakazi wa Shehia ya Kizimbani kwa  kukosa maji  ya safi na salama katika eneo hilo kwa kipindi cha muda mrefu.