January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nafasi za Kujitolea JKT zatangazwa,yasisitizwa nafasi hizo ni bure

Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

JESHI la Kujenga Taifa(JKT)limetangaza nafasi za kujitolea   mwaka 2023 kwa vijana wote kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wenye sifa za kujiunga na Jeshi  hilo huku ikisisitizwa kuwa nafasi hizo ni bure.

  Akizungumza na waandishi wa Habari Makao Makuu ya Jeshi hilo  Chamwino mkoani Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele ,Mkuu wa Tawi la Utawala wa  JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amewataka waombaji wa nafasi hizo kutorubuniwa na  mtu yeyote kwa kumpa fedha ili kufanikisha yeye kupata nafasi za kujiunga na mafunzo hayo kwa vijana wa kujitolea. 

“Kumekuwa na wimbi la utapeli unaoendeshwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwaomba fedha vijana wanaoomba nafasi hizo,naomba niwaambie nafasi hizi haziuzwi ni bure hivyo kila mmoja aombe sehemu husika zilizotolewa na JKT,” amesema

Amewataka  watakaopata nafasi hizo  kuripoti katika kambi za JKT kuanzia Septemba 26 hadi 29 Mwaka huu huku akisema  usaili utaanza Agosti 28, mwaka huu kupitia Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema utaratibu wa vijana kuomba na hatimaye kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo unaratibiwa na ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambako mwombaji anatoka.

Aidha amesisitiza kuwa,kwa Vijana watakaopata fursa hiyo kuwa JKT  halitoi ajira, wala kuwatafutia ajira kwenye asasi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali au vyombo vya ulinzi na Usalama. 

Akitaja sifa kwa waombaji wa darasa la Saba Brigedia Jenerali Mabena amesema  , awe na umri wa miaka 16 hadi 18 ambao wamemaliza elimu ya msingi kuanzia mwaka 2020, 2021, 2022 na awe na chati halisi cha kumaliza elimu ya msingi.

Aidha kwa vijana wenye elimu ya kidato cha nne umri usiwe zaidi ya miaka 20  na waliomaliza elimu ya Sekondari  kuanzia mwaka 2020, 2021, 2022 na awe na cheti halisi cha kumaliza elimu ya sekondari na cheti halisi cha matokeo ,na awe na ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi daraja la nne kwa  ufaulu wa alama kuanzia 26 hadi 32.

Amesema vijana wenye elimu ya kidato cha sita umri usiwe Zaidi ya miaka 22 na awe amemaliza elimu ya Sekondari kuanzia mwaka 2020, 2021, 2022 na awe na cheti halisi cha kumaliza elimu ya sekondari , cheti halisi cha matokeo na awe na ufaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la nne.

Kwa upande wa vijana wenye elimu ya stashahada umri usiwe zaidi ya miaka 25 awe na vyeti vya Sekondari na chuo, na vijana wenye shahada umri usiwe zaidi ya miaka 30 na awe na vyeti vya sekondari na chuo, na vijana wenye elimu ya shahada ya uzamili umri usiwe Zaidi ya miaka 30 awe na vyeti vya sekondari na cheti cha chuo.

 “Vijana watakaochaguliwa wanatakiwa kuja na vifaa kama bukta ya rangi ya dark blue, raba za michezo zenye rangi ya kijani au blue, shuka za kulalia rangi blue bahari, soksi rangi nyeusi, nguo za kuzuiabaridi watakaopangwa kwenye mikoa yenye baridi, flana ya rangi ya kijani kibichi yenye kola ya duara isiyo na maandishi” amesisitiza

Sifa za muombaji na maelekezo ya vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo vinapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz