Na Penina Malundo ,Timesmajira
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limeelezea dhamira yake kuhakikisha kuwa mafunzo ya ufundi na yale ya amali yanayotolewa kwenye vyuo na shule za sekondari za ufundi nchini yanazingatia viwango na ubora ili kuzalisha wahitimu wanaokubalika katika soko la ajira.
Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda, ameeleza hayo leo tarehe 19 Machi, 2025, wakati akichangia mada kuhusu mchango wa wahitimu wa ufundi stadi katika maendeleo ya jamii na uchumi, kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 30 ya VETA, linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Dkt.Lingwanda amesema matarajio ya Serikali ni kuwa na wahitimu wa ufundi na amali watakaochangia kikamilifu katika shughuli za uzalishaji kupitia ujuzi walioupata. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanyika tafiti za mara kwa mara katika sekta ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ili kuwezesha uandaaji wa mikakati madhubuti ya kuboresha utoaji mafunzo kulingana na mahitaji ya viwanda na soko la ajira kwa ujumla.
“Tafiti za mara kwa mara zitasaidia kutoa taarifa sahihi kuhusu mahitaji ya soko la ajira na kutoa mrejesho kuhusu wahitimu wa ufundi, hivyo kuboresha utoaji mafunzo kwenye vyuo vyetu,” amesema Dkt.Lingwanda

Dkt.Lingwanda amewahakikishia wadau kuwa NACTVET itaendelea kushirikiana nao katika kuimarisha utoaji mafunzo ya ufundi na kuzalisha wahitimu wenye sifa watakaoweza kuajirika na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Aidha amesema taasisi yao inatarajia kuja na mfumo maalum wa Kieletronic utakaochakata takwimu na taarifa mbalimbali zinazotoka katika Vyuo vya Ufundi na Ufundi Stadi,Wahitimu,Waajili na wale wanaojiajili.

Amesema awali walikuwa wakitumia njia ya kawaida katika kukusanya takwimu na taarifa hizo hivyo baada ya mfumo huo kuja utaweza kuwarahisishia kazi yao kwa urahisi na ufanisi.
“Jukumu letu kama baraza ni kuhakikisha tunakuwa na taarifa au takwimu ambazo ni sawa ambazo zitaweza kufanyiwa kazi na watafiti pindi wanataka kujua mambo mbalimbali ya wahitimu ikiwemo walioajiliwa au waliojiajiri wapo wangapi hadi sasa.

”Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia bajeti ya nyongeza mwaka huu ambayo baadhi ya kiasi cha fedha hizo tutatumia katika kutengeneza mfumo huo,”amesema.
Aidha Dkt.Lingwanda amesema mfumo huu utaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukusanya hizo takwimu na kama watahitaji kutembelea taasisi hizo au wahitimu hao ni pale watakapolazimika kwenda kufanya uhakiki.
”Mfumo huu utatusaidia kupata taarifa na takwimu hadi kwa wazazi ambao watoto wao wamesoma katika taasisi ya vyuo hivyo vya fundi na ufundi stadi,walimu,vyuo vyenyewe pamoja na wahitimu katika kujua mambo mbalimbali.
”Kwa sasa takwimu tunazo lakini tunataka kukusanya nyingi zaidi ikiwemo kutoka kwa wahitimu wenyewe hadi waajili,watuambie mawazo yao baada ya kuhitimu mafunzo na pia tutawafikia hadi wazazi itatusaidia katika kufanya maamuzi,”amesisitiza.
More Stories
Wasira awataka Wenyeviti CCM kuiga mfano Mkoa wa Mbeya
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,yajizatiti kuboresha uwezo wa Mawakili wa Serikali
MSD:Serikali inatekeleza mpango uchujaji wa damu