January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu waziri wa maji: Serikali  yatenga bllioni 2.8 miradi ya maji Wilaya ya Malinyi

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Morogoro

SERILALI imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji mitano ya maji katika wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro.

Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na Misegese, Itete Njiwa, Igawa,  Ngoheranga na Uchimbaji wa visima virefu 14  huku mradi wa maji Ngoheranga ukitarajiwa kutekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 kiasi cha Shilingi Milioni 641.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) wakati wa ziara ya siku mbili katika Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro yenye lengo la kukagua miradi ya maji sambamba na kuwatambulisha Wakandasi watano waliochaguliwa kutekeleza miradi ya maji katika Wilaya hiyo.

Mhandisi Mahundi amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi ya shilingi bilioni 3  zitatumika kwa ajili ya miradi mbalimbali katika Wilaya ya Malinyi.

Hata hivyo Naibu waziri huyo amesema ushirikiano baina yake na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na watumishi wa Wizara ya maji utaifanya Serikali kufikia malengo yake kwa nia ya kuwaondolea kadhia ya upatikanaji wa majisafi na salama.

Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza fedha nyingi katika miradi ya maji ilu kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata majisafi, salama na ya uhakika hii ni katika kutimiza ile azma ya kumtua mama ndoo kichwani.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Malinyi Mheshimiwa Antipas Mgungusi mbali ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maji kwa ujumla amewatoa hofu wananchi kwa namna walivyokumbukwa katika miradi mbalimbali ya maji hivyo wananchi kuendelea kuiamini Serikali.

 Mgungusi hakusita kuwapongeza Mawaziri na watumishi wote wa Wizara kwa namna wanavyochukua hatua za kusimamia utekelezwaji wa miradi ya maji nchini.