October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Mwinyi akisalimia wananchi.

Dkt. Mwinyi awaonya wanaojihusisha na magendo

Na Is-Haka Omar, Zanzibar

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka baadhi ya wananchi wa vijiji vya Uzi na Ng’ambwa vilivyopo Kusini Unguja wanaojihusisha na vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya na magendo kuacha mara moja na badala yake atawatafutia njia nyingine ya kuboresha maisha yao kwani vitendo hivyo vya kihalifu haviwezi kuwaletea maendeleo wananchi hao na vinaenda kinyume na sheria za nchi.

Dkt. Mwinyi ametoa wito huo kwenye mkutano wake wa kampeni, ambapo alitumia nafasi hiyo pia kumnadi mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Magufuli, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

Amesema, CCM itahakikisha utekelezaji wake wa ilani unasaidia kufanikisha malengo ya Serikali kupitia vijiji hivyo na aliwasihi wananchi wawe wavulivu na wewnye maono ya ushindi kwa kuwa na maisha bora kuliko awali.

Dhamira yake ya kuwania kiti hicho cha urais ni kuleta maendeleo kwa wananchi wote na kwa upande wa vijiji, ataimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii, miundombinu ya kisasa ya barabara na umeme,ujenzi wa miradi ya kiuchumi yakiwemo masoko na maduka ya kuwapunguzia wananchi kwenda mbali kutafuta huduma.

Endapa atachaguliwa na wananchi kwa kura nyingi na kuwa rais wa Zanzibar atahakikisha wananchi hao wanafanya kazi halali katika sekta zinazotambulika, huku vijana akiwapatia fursa za kujipatia kipato halali.

Ahadi hizo amezitoa katika mwendelezo wa ziara zake za kukutana na wananchi wa vijiji mbalimbali vilivyopo Wilaya ya Kati Unguja.

Baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo wamekuwa wakijihusisha na vitendo visivyofaa vya kuuza na kusambaza dawa za kulevya jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya nchi.

Amesema kuwa, Serikali ijayo ya awamu ya nane itavifanya vijiji hivyo kuwa miongoni mwa vijiji vya mfano kimaendeleo kwani wakisogezewa huduma za msingi za kijamii na kuboreshewa maisha yao kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wa ahadi, Dkt. Hussein Mwinyi amesema, atajenga hospitali ya kisasa ambayo itakuwa na huduma zote muhimu ikiwemo za mama na mtoto na upasuaji katika Kijiji cha Uzi na Ng’ambwa vilivyopo Kusini Unguja, Wilaya ya Kati kwani jiografia ya vijiji hivyo ili ufike ukitokea Unguja mjini ni lazima uvuke maji, ambapo yakipwa gari zinapita, yakijaa wakazi wanalazimika kuyasubiri hadi yaondoke.

“Nimetembea maeneo mengi na nimeahidi kutatua changamoto nyingi, lakini kama kuna kijiji kinahitaji kusaidiwa kutokana na mazingira yake yalivyo basi ni hiki.
Mgonjwa hawezi kufika kwa wakati upande wa pili kulingana na mazingira, hill nimelichukua na nitalifanyia kazi haraka iwezekanavyo” amesema Dkt. Mwinyi.

Pia atasimamia ujenzi wa barabara ya kutoka Unguja Ukuu mpaka Ng’ambwa yenye urefu wa kilomita 3.5 na daraja.

“Hili tayari limo katika ilani ya uchaguzi kilichobaki ni kutekeleza tu kuhusu njia ya ndani hilo ondoeni shaka nitahakikisha nalisimamia kumaliza aza hii ili muendelee na shughuli za kujitafytia riziki na maendeleo,”.

Ili vijiji hivyo viwe na maendeleo Dkt. Mwinyi amesema ni lazima kuwe na miundombinu imara kama daraja na barabara ili kutoathiri shughuli za maendeleo.

Kuhusu watu wenye ulemavu, Dkt. Mwinyi amewahakikishia kuwa ataendelea kuwasaidia kwa kuwapa virahisishi mwendo ili wajikwamue kimaisha kwani anajua katika maeneo ya mbali namna hiyo watendaji huwa hawafiki kufuatilia shughuli za maendeleo ikiwamo miradi.

“Nitakuwa wa kwanza kufuatilia Serikali yangu itakuwa haina watendaji wa kukaa maofisini, watu wote watatembea ili kuwatumikia wananchi ndio lengo langu kuu la kugombea nafasi hii,”.