Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Mzee Hassan Wakasuvi ambaye pia alikuwa Mlezi wa chama wa Mkoa wa Arusha amefariki dunia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa Balozi Dkt Batilda Burian amethibitisha kutokea kifo hicho na kubainisha kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuondokewa na Kiongozi wao.
Amesema kuwa marehemu Wakasuvi amepatwa na umauti huo baada ya kuanguka akiwa ofisini kwake ambapo Viongozi na WanaCCM waliokuwepo Ofisini hapo walimkimbiza Hispitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Kitete kwa ajili ya matibabu zaidi lakini haikusaidia kuokoa maisha yake.
Ameeleza kuwa marehemu alikuwa Kiongozi makini sana na nguzo ya chama katika Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
RC amebainisha kuwa saa 1 kabla ya kifo chake aliongea naye kwa njia ya simu ambapo alikuwa anampa taarifa ya utekelezaji masuala mbalimbali yahusuyo wananchi wa Mkoa huo na hakumweleza kama alikuwa na tatizo lolote la kiafya.
‘Tumepoteza Kiongozi makini, kipenzi cha watu, aliyekipigania chama usiku na mchana na kukiimarisha ndani na nje,’ amesema.
RC alibainisha kuwa amepokea taarifa hiyo ya ya kusikitisha akiwa safarini na sasa yuko njiani anarudi Tabora kwa ajili ya kukutana Wanafamilia na Viongozi wa Chama ili kuandaa taatibu zingine na kuutaarifu umma ratiba ya mazishi yake.
‘Natoa pole sana kwa Viongozi wa Chama na Serikali, Wakazi wa Mkoa wa Tabora, wanaCCM na jamii kwa ujumla kwa kuondokewa na Kiongozi wetu, Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,’ alieleza
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete Dkt Mark Waziri ameeleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha kifo hicho ni mshituko wa moyo (heart attack) na pia marehemu alikuwa na tatizo la shinikizo la damu (blood pressure).
More Stories
Sherehe Miaka 61 ya Mapinduzi Zanzibar zafana
Simbachawene:Waombaji wa ajira jiungeni na Mfumo wa Ajira Portal
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050