Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online,Rorya
MWENYEKITI mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara,Gerald Ng’ong’a amepiga marufuku madiwani katika halmashauri hiyo kulipwa posho zao kwa fedha taslimu na badala yake malipo yote yapitie kwenye akaunti zao za benki.
Mbali ya posho za madiwani pia mwenyekiti huyo ameagiza makusanyo yote ya mapato ya Halmashauri yakusanywe kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ambapo kila mtu anayelipa malipo yoyote ya halmashauri apatiwe namba ya malipo (control number) ili akalipie benki badala ya kulipa fedha taslimu.
Ng’ong’a ametoa agizo hilo muda mfupi mara baada ya kuchaguliwa rasmi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya kwa kupata kura zote 35 za ndiyo baada ya mpinzani wake katika nafasi hiyo, Khalfan Abdul kutoka Chama cha ACT-Wazalendo kujitoa.
“Ndugu zangu baada ya kukabidhiwa jukumu la kuiongoza Halmashauri yetu, tukumbuke mambo mawili ya kuanza nayo kwa haraka haraka, jambo la kwanza ni suala la ukusanyaji wa mapato ya halmashauri, bila ya kuwa na fedha, tuelewe shughuli zetu nyingi za kimaendeleo zitakwama,”
“Kuna suala la ubadhirifu limezungumzwa hapa, Mkurugenzi na timu yako niwaombe kuanzia sasa malipo yote ya vikao vya waheshimiwa madiwani yapitie benki, madiwani wote wawasilishe kwako namba zao za akaunti za benki, hata kama ni posho ya shilingi elfu kumi, diwani akutane nayo benki,” ameeleza Ng’ong’a.
Mwenyekiti huyo ameagiza wakusanya mapato wote katika Halmashauri hiyo waachane na utaratibu wa kupokea fedha taslimu na kutoa stakabadhi za karatasi na badala yake wawe wanatoa namba za malipo (control number) ili mlipaji akalipe fedha hizo benki au kwenye taasisi nyingine za kifedha.
Amesema kwa kutumia mfumo wa kielekroniki katika ulipaji wa fedha na ukusanyaji wa mapato utasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti mianya ya ubadhirifu wa fedha za Halmashauri na kwamba kupatikana kwa fedha nyingi kutasaidia Halmashauri hiyo kufikia malengo iliyojiwekea katika utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga amewapongeza madiwani wote kwa kuchaguliwa kwao kuiongoza Halmashauri hiyo ambapo hata hivyo amewaomba waweke pembeni tofauti walizokuwa nazo kipindi cha kampeni na washikamane katika kuijenga Halmashauri yao.
Odunga amesema mara baada ya kukamilika kwa shughuli za uchaguzi kila mmoja wao anapaswa kuanza kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi kwa lengo la kuwaletea maendeleo na kwamba kipindi cha kupiga porojo hivi sasa hakipo tena.
“Mheshimiwa mwenyekiti nikupongeze wewe na makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuiongoza Halmashauri yetu ya Rorya, Ofisi yangu itakuwa bega kwa bega nanyi na haitobagua mtu ye yote hata kama ni diwani anayetokana na chama cha upinzani, uchaguzi umepita, hivyo tujikite kwenye kuwaletea maendeleo wananchi wetu.
“Kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kutekeleza ahadi tulizozitoa kwa wananchi na kuanza na vipaumbele muhimu ambavyo hata Rais wetu, Dkt. John Magufuli aliviainisha alipokuwa akizindua Bunge letu hivi karibuni, na hapa kwetu tuna mambo matatu ya kuzingatia ikiwemo suala la elimu, tuhakikishe tunaongeza vyumba vya madarasa,” ameeleza Odunga.
Anafafanua mkuu huyo alisema Halmashauri ya Rorya mpaka hivi sasa ina upungufu wa vyumba vya madarasa 129 katika shule zake za msingi na sekondari na kwamba juhudi kubwa zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wake ambapo amewashukuru wale wote waliokubali kuchangia ujenzi wa vyumba hivyo.
“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha agizo lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa linatelekezwa ili ifikapo Februari 28, mwakani ujenzi wa vyumba hivyo uwe umekamilika na kuwezesha watoto wote wa darasa la saba waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza waweze kupata nafasi za kuanza masomo,” ameeleza Odunga.
Katika hatua nyingine mkuu huyo ametoa siku 90 kwa watumishi wote wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya wanaoishi nje ya Makao Makuu ya Halmashauri hiyo wahakikishe wawe wamehamia katika eneo la halmashauri vinginevyo hatosita kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Odunga amesema amebaini kitendo cha watumishi kuishi nje ya makao makuu ya Halmashauri ni moja ya sababu za wengi wao kuchelewa kufika kazini kwa wakati na hivyo kusababisha wananchi wengi kutohudumiwa ipasavyo ambapo pia amepiga marufuku kauli za watumishi kuwaambia wananchi, ‘…Njoo kesho’
More Stories
Serikali yahimiza wananchi kutembelea vivutio vya utalii
Magunia ya kufungia tumbaku yakamatwa
Madereva 16,Mwanza wafungiwa leseni ya udereva