Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Mbozi.
WAKULIMA na wakazi wa kata nne za Iyula, Idiwili, Hezya, Nyimbili na Mlangali katika Wilaya ya Mbozi wameishukuru serikali kwa kuanza ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Ilolo – Ndolezi yenye urefu wa Kilometa 11.01.
Barabara hiyo ambayo pia inaelekea katika eneo la utalii la kimondo katika kata ya Ndolezi ujenzi wake unagharimu shilingi 6,465,597,070 , imewekewa jiwe la msingi leo Septemba 4, 2023 na kiongizi wa mbio za mwenge kitaifa 2023,Abdalla Shaibu Kaim.
Wananchi mbalimbali wakizungumza kabla na baada ya barabara hiyo kuzunduliwa walielezea manufaa ya barabara hiyo kwa kuwa inaunganisha eneo la mashamba, masoko pamoja na maghala ya kuhifadhi mazao na pembejeo za kilimo.
Naye mbunge wa jimbo la Vwawa, Japhet Hasunga, amesema barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa itarahisisha usafirishaji wa pembejeo za kilimo na mazao kutoka mashambani kwenda maghala , viwandani na masoko kutoka kwa wakulima na wakazi wa kata hizo za Iyula, Idiwili, Hezya, Nyimbili na Mlangali.
Awali akisoma taarifa juu ya ujenzi wa barabara hiyo ya Ilolo – Ndolezi kwa niaba ya Kaimu Meneja wa Wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Fred Mlowe amesema ujenzi wa barabara hiyo ambao pia unafadhiliwa na jumuiya ya umoja wa ulaya chini ya ya mradi wa Agri-Connect umefikia asilimia 25 .
Mhandisi Mlowe amesema tayari Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambaye ni kampuni ya IRA na Globali Link za Mkoani Mbeya chini ya Mhandisi mshauri kampuni ya Inter ya Jijini Dar es salaam amelipwa kiasi cha shilingi 981,460,210 ambazo ni sawa na asilimia 15.17.
Mhandisi Mlowe ameeleza kuwa mradi huo ulianza utekelezaji wake Aprili 4, 2023 na unatarajia kukamilika ifikapo Aprili 3 , 2024.
Kwa upande wake, kiongozi wa mbio za mwenge 2023, akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua kisha kuweka jiwe la msingi amewataka watendaji na viongozi wa serikali wilayani Mbozi kuhakikisha mradi huo unajengwa kwa kiwango na gharama zilizowekwa na kwamba kila anayehusiaka kwenye mradi huo anapaswa kutanguliza uzalendo kwa maslahi ya Taifa.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba