Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza unatarajia kupokelewa Julai 17,2022 huku ukipita katika Kata 6 kati ya 18 zilizopo katika wilaya hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi,wakati akizindua kampeni ya hamasa ya Mwenge wa Uhuru na elimu ya sensa ya watu na makazi 2022 kwa Wilaya hiyo uliofanyika katika uwanja mkongwe wa Nyamagana uliopo wilayani humo.
Makilagi ameeleza kuwa,Wilaya hiyo itapokea Mwenge wa Uhuru Julai 17 mwaka huu ambapo utapokelewa eneo la Kamanga Ferry ukitokea Wilaya ya Ukerewe na utakimbizwa katika Kata 6 wilayani humo ikiwemo ya Nyamagana,Igogo,Mkuyuni,Nyegezi,Mkolani na Buhongwa.
Ameeleza kuwa katika Kata ya Nyamagana Mwenge utazindua mradi wa vijana,Igogo wataenda kuangalia mradi wa maji safi na salama na mradi wa maji taka ulioboreshwa kwa lengo la kupeleka maji milimani na majitaka zamani ambayo yalikuwa yanapelekwa ziwani sasa waneanda mfumo rasmi ambapo yatapelekwa kwenye maeneo ambayo yametengwa rasmi kwa lengo la kuboresha mazingira kuwaepusha wananchi na kutoleta mlipuko wa magonjwa katika Wilaya hiyo.
Kata ya Mkuyuni Mwenge huo utazindua madarasa yalijengwa kwa mfumo wa ghorofa ambayo Rais aliwapatia zaidi ya bilioni 1.9 na wakaongezea zaidi ya bilioni 2 fedha za mapato ya ndani pamoja na wahisani wanaendelea kujenga na ambapo yakikamilika watakuwa na madarasa 260 kwa mwaka mmoja lengo ikiwa ni watoto wasikose darasa hata mmoja kwa ajili ya kuendelea kufundishiwa.
Buhongwa watakwenda kuzindua kituo cha Afya ambacho Rais aliwapatia milioni 500 fedha zilizotokana na tozo za miamala ya simu walizotoa wananchi kisha wataenda CRDB kupitia mradi wa mtu binafsi kuzindua benki.
Hivyo ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika siku hiyo ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwani inakuja kukagua na kuangalia miradi ili kulinganisha thamani ya fedha iliotumika kwenye miradi kama inaendana na utekelezaji wake.
Aidha ameeleza kuwa Wilaya ya Nyamagana pia itashiriki zoezi la sensa ya watu na makazi na ni zoezi muhimu kwa taifa ili serikali iweze kupanga mipango mbalimbali ya kusogeza huduma karibu kwa jamii hivyo wananchi washiriki katika zoezi hilo.
“Lengo la kuwaita hapa kwanza ni kushiriki mazoezi ambayo ni afya, upendo na ushirikiano na yanatuleta pamoja kama watanzania,kuonesha Nyamagana tupo tayari kwa zoezi la sensa vikundi hivi mtusaidie kupeleka ujumbe kwa wananchi kuwa ifikapo Agousti 23, kila mtu akubali kuhesabiwa pasipo na vikwazo na kufanya uzinduzi wa maandalizi ya Mwenge wa Uhuru katika Wilaya yetu ambao umebeba ujumbe wa sensa ya watu na makazi katika taifa letu,”ameeleza Makilagi.
Mratibu wa sensa ya watu na makazi Wilaya ya Nyamagana Constantine Ruhinda, ameeleza kuwa tangu Tanganyika imepata Uhuru sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 na Watanzania tulikuwa milioni 12 ila sasa tunakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 50.
Serikali inatumia gharama kubwa kufanya zoezi la sensa kwani ni msingi wa maendeleo bila ya kuwa na idadi ya watu hauwezi kupanga bajeti ya watu wake kulingana na shughuli na rasilimali zilizopo.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Florah Magabe,ameiomba jamii kutowaficha Watoto wenye ulemavu wakati wa zoezi la sensa.
“Watoto wenye ulemavu nao wapate fursa ya kuhesabiwa ili serikali inapoweka bajeti yao iweze kuwafikia na kuwapatia mahitaji yao,”.
More Stories
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji
Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba