September 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wa uhuru kuzindua miradi ya zaidi ya bil.2.8 Tanganyika

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Tanganyika.

SERIKALI ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi imesema Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 utakimbizwa kuanzia September 13, 2024 na kuzidua miradi yenye thamani ya fedha zaidi ya Bil 2.8 wilayani humo.

Amesema hayo Mkuu wa wilaya hiyo, Onesmo Buswelu leo September 9, 2024 ofisini kwake kata ya Majalila wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamilika maandalizi ya kupokea Mwenge huo.

“Nia ni kufahamisha umma kwamba tupo tayari kuupokea,kuulaki kwa furaha na shangwe Mwenge wa Uhuru ambao utawasili asubuhi katika viwanja vya shule ya sekondari Kabungu na baada ya kukimbizwa utakwenda kukesha viwanja vya shule ya msingi Mpandandogo” Amesema.

Mwenge wa Uhuru ukiwa katika wilaya ya Tanganyika utakimbizwa katika kata za Kabungu,Mnyagala,Sibwesa,Kasekese, Mpandandogo na Tongwe na baadaye Septermber 14, 2024 kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

Buswelu ameweka wazi kuwa licha ya Mwenge huo kukimbizwa katika kata hizo sita pia utazidua, kuweka Mawe ya Msingi na kutembelea miradi mbalimbali.

Miradi hiyo ni pamoja na kuzindua mradi wa maji Mnyagala wenye thamani ya Bil 1.357 fedha kutoka serikali kuu, Kutembelea kiwanda cha kukoboa mpunga na kuhifadhi mazao cha Flamingo food Co Ltd Ikaka chenye gharama ya fedha Mil 700 kutoka chanzo binafsi.

Aidha utatembelea shamba la miti Zahanati ya Kagunga thamani yake ni Mil 900, Kuzindua Zahanati ya Kagunga thamani yake Mil 408.244 na Kutembelea jengo la wagonjwa wa nje (OPD) kituo cha afya Sibwesa thamani yake ni Mil 216.285 ambapo fedha zote hizo ni kutoka mapato ya ndani.

Mkuu wa wilaya hiyo,amesema miradi mingine ni kuweka Jiwe la msingi bweni la wasichana shule ya sekondari Majalila wenye thamani ya Mil 170, Kutembelea shughuli za kikundi cha vijana Gift Kasekese wenye thamani ya Mil 25 na kuzindua klabu ya mapambano dhidi ya rushwa shule ya sekondari Sibwesa wenye thamani ya Mil 1.33 zote kutoka mapato ya ndani.

Vilevile amesema katika kukabiliana na udumavu wa watoto unaosababishwa na lishe duni,Mwenge wa Uhuru utazindua klabu ya lishe katika shule ya sekondari Sibwesa uligharimu Mil 1.3 fedha kutoka mapato ya ndani.

Kutokana na umuhimu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa wenye ujumbe “ Tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ujenzi wa taifa endelevu” wilaya ya Tanganyika katika uwanja wa shule ya msingi Mpandandogo utafanya kongamano lenye vijana zaidi ya 1000 kwenye mkesha huo na kutoa mada mbalimbali.

Mratibu wa kongamano la vijana wa wilaya hiyo,Otman Kasamya amesema Mwenge wa Uhuru umewataka kuandaa kongamano la vijana ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa.

Mada hizo ni pamoja na Uzalendo na Falsafa ya Mwenge wa Uhuru, Fursa za uwezeshwaji wananchi kiuchumi, Fursa za kilimo na uzalishaji, Fursa za uvuvi na ufugaji, Maadili na makuzi na shughuli za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Hivyo amewaomba vijana wote wa ndani na nje ya wilaya hiyo kujitokeza kushiriki kongamano hilo ambalo litakuwa na tija kubwa katika kujenga uzalendo, kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na kufanya kazi kwa maendeleo yao na taifa.