Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online Mwanza
Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Mkoa wa Mwanza umepokea kiasi cha zaidi ya bilioni 3.2(3,213,430,392.23), kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 40 ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu,afya na ajira za muda.
Huku katika kipindi cha miaka mitano Mkoa unatarajia kupokea kiasi cha zaidi ya bilioni 24.3(24,395,865,000) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kupunguza umaskini.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,wakati akifungua kikao kazi cha kujengeana uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa miradi ya kupunguza umaskini awamu ya nne(TPRP IV) katika mpango wa TASAF Mkoa wa Mwanza kilichofanyika mkoani hapa.Mhandisi Gabriel, amesema kati ya miradi hiyo 23 ni miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu,miradi ya afya 16 pamoja na mradi wa ajira za muda 1.
“Matarajio yangu ni kuwa mradi huu wa awamu ya nne utawezesha jamii kupata mafanikio ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya na elimu hasa katika kuwezesha watoto chini ya miaka mitano kuhudhuria kliniki na wanafunzi kuhudhuria shuleni,” amesema Mhandisi Gabriel.
Pia amewasisitiza, viongozi na wataalamu wote kuzingatia sheria,kanuni, taratibu na miongozo wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na usimamizi thabiti ili thamani ya fedha itakayotumika iendane na ubora wa miradi hiyo.
“Wakati wote wa utekelezaji wa miradi hii ni vyema kuhakikisha ubora wa miradi na thamani ya fedha ya miradi ionekane,pia nichukue fursa hii kuipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kwa azma iliopo ya kuinua kipato cha kaya zenye changamoto ya kiuchumi,”amesema Mhandisi Gabriel.
Kwa upande wake Katibu Tawala Masidizi- Mipango na Uratibu Mkoa wa Mwanza Joachim Otaru,amesema zoezi la uibuaji wa miradi ya kupunguza umaskini awamu ya nne(TPRP IV), ambapo jumla ya miradi 104 imeibuliwa na kupitishwa na Wizara kwa ajili ya utekelezaji.
Ambapo amesema kati ya miradi hiyo 31 ni ya afya,49 elimu na 24 ni miradi ya kutoa ajira za muda(PWP),jumla miradi hiyo itagharimu kiasi cha zaidi ya bilioni 7.8(7,845,316,205.24).
“Miradi iliopokea fedha hadi sasa,Mkoa umepokea jumla ya bilioni 3.2(3,213,430,392.23), kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 40 ya ujenzi wa miundombinu ya elimu 23,afya 16 na mradi wa ajira za muda 1,”amesema Otaru.
Naye Mratibu wa TASAF Mkoa wa Mwanza Monica Mahundi, amesema Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa mitano inayotekeleza miradi ya kupunguza umaskini awamu ya nne.
“Mkoa wa Mwanza jumla tumepokea fedha zaidi ya bilioni 3.2 ya kutekeleza miradi 40 ikiwa na maana ya miradi mitano kwa kila Halmashauri zilizopo mkoani hapa,ambayo inaanza utekelezaji muda si mrefu kuanzia sasa,” amesema Mahundi.
Amesema,kwa ujumla Mkoa wamejipanga kutekeleza miradi hiyo ipasavyo na kwa ufanisi na kufuata maelekezo na taratibu zilizotolewa.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba