Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
IMEELEZWA kuwa zaidi ya Sh. bilioni 1.2 (1,234,440,000) zitatumika kulipa madeni na mkataba wa dharura wa mwaka wa fedha wa 2019/20 kama ilivyoelekezwa na Serikali.
Fedha hizo zitatoka katika bajeti iliyoidhinishwa kwa Mkoa wa Mwanza kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambazo ni zaidi ya Sh. bilioni 14.9 (14,987,226,000).
Miongoni mwa fedha hizo, bajeti kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara kwa mwaka 2020 hadi 2021 ni zaidi ya bilioni 13.7 (13,752.786,000).
Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Vedastus Maribe wakati wa kikao Kazi cha kwanza cha Bodi ya barabara ya Mkoa wa Mwanza kwa mwaka wa fedha 2020/21 kilichofanyika mkoani hapa.
Mhandisi Maribe amesema, mbali na bajeti hiyo pia zaidi ya bilioni 3.4 (3,452,560 .000) zimeidhinishwa kutoka mfuko wa maendeleo kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara,madaraja pamoja na miradi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mkoani Mwanza.
Akizungumzia utekelezaji wa Kazi na matengenezo ya barabara, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(TARURA) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Gaston Paschal amesema, wanashughulikia matengenezo ya barabara za Mjini na vijijini katika Halmashauri za Magu, Misungwi, Ukerewe, Buchosa, Sengerema, Kwimba, Ilemela na jiji la Mwanza hivyo kwa mwaka wa fedha 2020 hadi 2021 kwa Mkoa wa Mwanza wamepangiwa bilioni 11.2( 11,271,973,781.87)
Amesema, Halmashauri zote zina mtandao wa barabara jumla ya kilometa 8628.039 hadi Disemba 2020, na kulingana na uthibitisho wa mtandao wa Wizara ya ujenzi uchukuzi na mawasiliano , nje ya mtandao huo barabara za lami ni Kilometa 72.89, barabara za changarawe ni kilometa 1286.16, barabara za udongo ni kilometa 7253.156 , zege zikiwa kilometa 4.795 na za mawe zikiwa ni kilometa 11.03.
Akielezea matatizo yanayowasibu, Mhandisi huyo amesema, kwa asilimia fulani kitendo cha wananchi kufanya shughuli za kibinadamu kama kilimo katika maeneo ya hifadhi pamoja na kiwango kidogo cha fedha za matengenezo ukilinganisha na hali halisi ya mahitaji ya matengenezo ya barabara.
“Wizi na hujuma za alama za barabarani, makalavati, vyuma vya madaraja, taa za barabarani, betri , waya za umeme , uchimbaji wa wananchi kupitisha mifugo barabarani, magari mazito kutumia barabara za viwango vidogo hayo yote ni matatizo” amesema Paschal.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akifungua kikao hicho alisema, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo Mwanza itakuwa na sura mpya na tofauti kutokana na viongozi waliopo kwa sasa hivyo mshikamano unahitajika ili kuimarisha miundombinu ya mkoa kwani serikali imetowa fedha nyingi za kutekeleza miradi mbalimbali.
Amesema kwa miaka mitano iliyopita, wamefanikiwa katika sekta ya elimu siri ya mafanikio hayo ni uchapakazi ,umoja na utendaji kazi wenye tija ambao ulichangia watoto wote waliochaguliwa walifanikiwa kujiunga na shule hivyo ata kwa walichangulia kwa mwaka huu lazima wote wataingia madarasani hivyo viongozi wote wafanye Kazi ili kuijenga nchi .
Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ameitaka TARURA kutoka ofisini na kutembelea maeneo ya wananchi kwani barabara nyingi ni za udongo hivyo mvua zinazoendelea kunyesha zimeharibu sana barabara.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum, Kalli na Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga wamesema, barabara ya Mahaha- Bariadi inaunganisha Mkoa wa Mwanza na Simiyu hivyo waliomba kujengwa kwa daraja ili kuweza kuunganisha mikoa hiyo na wananchi waweze kufanya shughuli zao za kimaendeleo .
Kwa upande wake Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni amesema, kuna madaraja matatu ambayo mvua ikinyesha maji yanapita juu yake hivyo kufanya wananchi wanapita kwa kudra za Mungu hivyo ameiomba TARURA kuyapa kipaumbele.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua