June 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwandishi wa habari achangia madawati ya shilingi milioni moja

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Kagera

MWANDISHI wa Habari,Mathias Canal amechangia Shilingi milioni moja ya madawati katika shule mpya ya msingi ya Kigasha ilipo katika jimbo la Karagwe mkoani Kagera.

Canal amesema amechangia madawati  hayo kutokana na juhudi zinazofanywa na Mbunge wa Jimbo la Karagwe Innocent Bashungwa katika kuimarisha sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Kigasha.

Amechangia madawati hayo mara baada ya kutembelea shule hiyo iliyopo katika kata ya Rugu, Tarafa ya Nyaishozi akiwa katika kazi ya kutembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya kujionea utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.

Amesema kuwa usimamizi wa ujenzi wa shule hiyo unaenda sambamba na serikali kupeleka walimu ambapo ametumia nafasi hiyo kumpongeza Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda kwa kuweka kipaumbele katika shule hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wa maeneo hayo wanapata elimu bora kama ilivyo katika maeneo mengine.

Kwa upande wake katibu wa Mbunge wa Jimbo la Karagwe Ivo Ndisanye amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule na upatikanaji wa walimu.

Pia kwa niaba ya Mbunge Innocent Bashungwa katibu huyo naye ameahidi kuchangia Shillingi Milioni tatu kwa ajili ya upatikanaji wa madawati ili kuimarisha ufanisi wa kujifunza.

“Niwapongeze wazazi na walezi wa wanafunzi katika kijiji hiki kwani kupitia nguvu yenu mmeweza kujenga madarasa mawili ambayo mbunge alitoa mabati kwa ajili ya kupaua,”amesema.