April 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ,awafunda mawakili wa serikali

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania,Hamza Johari amewaongoza Mawakili wa Serikali kushiriki katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali unaofanyika Jijini, Dodoma tarehe 14 hadi 15 Aprili, 2025.

Pia amewataka kujadili kwa kina masuala mbalimbali yanayohusu Chama chao pamoja na sekta ya Sheria kwa ujumla.

Akizungumza hayo leo Mkoani Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo,Johari alisema lengo la Mkutano huo ni kutoa fursa kwa wanachama wa Chama hicho cha mawakili wa Serikali kujadili mambo mbalimbali yanayohusu chama chao.

Amesema Mawakili hao wa Serikali wanatakiwa  kuendelea kutekeleza majukumu yao vizuri ili kuweza kuifikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Aidha amewataka Mawakili hao kuishi kwa kuzingatia kauli mbiu ya mkutano huo inayosema “Utawala wa Sheria katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali, ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”.

“Kauli mbiu yetu ya mwaka huu imejielekeza kwenye Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 ambapo ili iweze kufikiwa ni dira hii tunatakiwa kuwa na proper legal framework na sisi tunataka kuwa facilitator wa kulifikisha taifa huko,”amesema.

Awali, akimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Samwel Maneno amewahakikishia Mawakili wa Serikali kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Mawakili wa Serikali wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa ujasiri na ulinzi mkubwa bila kuteteleka.

”Tutahakikisha kila Mwanasheria kule aliko anatekeleza majukumu yake kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na milango ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu iko wazi wakati wowote ,”amesema

Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,Shaaban Ramadhan Abdalla ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania kwa kuialika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kuja kuhudhuria Mkutano huo huku akikipongeza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kuendelea kuwasimamia vizuri Mawakili wa Serikali.

Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali umeanza Aprili 14,2025 kwa Mawakili wa Serikali kupokea taarifa mbalimbali zinazohusu chama hicho na Mkutano utaendelea hadi Aprili 15, 2025 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Mashaka Biteko.

Kupitia mkutano huo Mawakili hao watapata fursa ya kufanya uchaguzi kwa kuwachagua viongozi mbalimbali wa kukiongoza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja.